Watafiti kutatua changamoto mabadiliko tabia nchi
WATAFITI nchini wametakiwa kuunda timu ya watafiti waliobobea vizuri kwenye maeneo yao, ili kuandika andiko linalolenga kutatua changamoto zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia ( Costech), Dk Amos Nungu amesema hayo alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu mwito uliotolewa na tume hiyo wa kualika watafiti nchini kuandika andiko la utafiti jumuishi.
“Mabadiliko ya tabianchi yanaathiri sekta zote. Tabianchi ni mtambuka masuala haya yanaathiri kilimo, maji na maeneo mengine,, hivyo ni vema kuwa na timu ya watafiti kutoka kwenye nyanja tofauti tofauti” amesema.
Amesema kupitia timu hiyo ya watafiti itawezesha kufanya tafiti zenye tija na k kuleta suluhu na uelewa wa changamoto zitokanazo na mabadiliko ya tabia nchi.
” Mwito huu umewataka pia watafiti waeleze ni kwa jinsi gani teknolojia watakazokuja nazo zitawafikia wananchi na jinsi gani tafiti zao zitachangia katika kuboresha sera zetu,” amesema.
Amesema kupitia mwito huo miradi itakayofadhiliwa ni mikubwa ambapo kila mradi unategemewa kugharamiwa kwa kati ya takribani sh milioni 220 hadi 600 kwa muda wa miaka minne.
” Ili kuhakikisha watafiti wanauelewa vizuri mwito huu, tume imeandaa warsha itakayofanyika kwa njia ya mtandao kesho Februari mosi.
” Lengo la warsha hii ni kujenga ufahamu na uelewa zaidi kwa watafiti wetu ili waweze kuandaa maandiko mazuri na shindani,” amesema.
Naye Ofisa Mratibu Mwandamizi wa Utafiti Costech, Neema Tindamanyire amewataka watafiti wote kutumia fursa hiyo na kujisajili kwa njia ya mtandao ili waweze kuhudhuria warsha na kupata fursa ya kuuliza maswali na kueleza changamoto walizonazo katika uandaaji wa maandiko yao,” alisema.
Oktoba mwaka jana tume ilisaini makubaliano na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Nchini Norway ( Norad), kwa ajili ya kutekeleza program ya utafiti wa mabadiliko ya tabianchi kwa miaka mitano ijayo.