Watafiti walivyobaini makubwa kwenye ‘mti maziwa’

UDAR ES SALAAM; MITISHAMBA ni mimea inayothaminiwa kama dawa. Katika matumizi ya dawa inawezekana kutumia sehemu yoyote ya mmea ikiwa ni pamoja na majani, mizizi, maua, mbegu, gundi, maganda ya mizizi, maganda ya ndani, nafaka na mara nyingine matunda au sehemu nyingine za mmea.

Robinson Mdegela ni Profesa kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Idara ya Tiba ya Wanyama na Afya ya Jamii, ambaye amejikita katika mazingira ya utafiti wa mazao ya miti dawa.

Profesa Mdegela anasema Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech), imemwezesha kupata takriban Sh milioni 100 kwenye miradi miwili, ambayo imesaidia kufanya utafiti wa kufuatilia dawa zinazotokana na miti, hasa asilia.

Lakini pia kujua namna gani hizo dawa zinavyoweza kutibu magonjwa kwa binadamu na wanyama, ikiwa ni pamoja na kuangalia changamoto za usalama wa dawa.

“Kwenye miradi hii miwili tuliyoifanya, shabaha na lengo kubwa ilikuwa ni kutoka katika hali ya kuonekana mazao ya miti dawa yanadharauliwa na kuyaongezea thamani, kwa kujua uhalisia hasa katika nyanja za kisayansi kuona kama kweli mazao hayo yanafanya kazi katika ubora unaostahili,” anasema.

Anaeleza walipoanza utafiti wa dawa katika miti ya asili waligundua soko lipo, lakini dawa hizo zinadharauliwa, kwamba kwa wale waliopo vijijini ambako miti hiyo ya dawa inapatikana huwa hawapati kipato kinachowastahili kwa kuwa dawa zinadharaulika na kipato kinakuwa kidogo.

“Tukatamani tufanye mradi utakaoboresha hayo mazao ili wanaojihusisha katika mnyororo wa thamani waweze kupata kipato kizuri.

“Tulianza kwa kuwa na andiko mradi na Costech walitufadhili kwa kutupatia fedha tukaanza kwenda vijijini kubaini uelewa wa wananchi wetu na watu mbalimbali kuhusiana na thamani ya dawa au hiyo miti dawa na mazao yake,” anasema.

Kwa mujibu wa Profesa huyo, wananchi waliwapatia orodha kubwa ya miti na namna zinavyoandaliwa, na zinavyotumika, nao wakajaribu kuangalia kwa sababu magonjwa wanayopambana nayo yanatokana na vimelea vya magonjwa.

Vimelea hivyo viko katika kundi la virusi, bakteria, na fangasi. Vipo vimelea vinavyosababisha magonjwa ya tumbo kwa aina mbalimbali, minyoo na magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari na kansa.

“Ukienda mahali popote hata kama hakuna hospitali au kituo cha afya lazima utasikia watu wanasema kuna tiba ya ugonjwa fulani.

“Tulipata orodha ndefu sana ya miti inayotumika kama dawa, tusingeweza kuifanyia kazi kwa wakati mmoja, kwa hiyo tukachukua baadhi na tukajikita katika magonjwa ambayo yalionekana yanaleta shida zaidi katika jamii kwa sasa.

“Wapo walioonesha kuwa kuna miti inayotumika kutibu magonjwa ya binadamu na wanyama na sisi tukachagua mti mojawapo ujulikanao kama ‘mti maziwa’,” anasema.

Anasema aina hiyo ya mti maziwa unaweza kutibu magonjwa ya ng’ombe na kuku. Hivyo waliitumia miti hiyo kama walivyoelekezwa kuona kama inaweza kutibu magonjwa ya kuku kama mdondo unaosababishwa na virusi.

Anasema katika huo utafiti walivyotibu kuku waliona mabadiliko makubwa kama kuku, lakini kuna namna walivyojaribu mayai kwa kuambukiza mayai kwa virusi halafu wanaweka dawa.

“Kilichotufurahisha ni kwamba mayai yaliyowekwa virusi bila dawa yalikufa, lakini mayai yaliyowekwa virusi tukaweka na dawa ambayo tuliijaribu vifaranga vilipona,” anasema.

Utafiti huo wa mayai ukawapa nafasi ya kutafiti zaidi mti maziwa huo. Katika mti huo wananchi walieleza kuwa unatibu kifua kikuu walipofuatilia wakagundua kwa namna fulani inasaidia watu wenye magonjwa ya kifua.

“Basi ikatupa nafasi ya kutafiti zaidi, wengine walisema inatibu magonjwa, kwani kama imeua virusi kwa kuku basi wakasema ingeweza kuua na magonjwa yanayosabibishwa na virusi kwa binadamu,” anasema.

Anasema kutokana na tafiti zao kwa wanyama ilibainika kuwa ni kweli katika huo mti waliokuwa wameamua kuutafiti ulithibitika kwamba unaweza kuua virusi, na kwa sababu ilidhihirika kuwa huo mti unatibu magonjwa yanayosabishwa na virusi vya binadam, waliona wajaribu kufuatilia pia upande wa virusi.

Baada ya kupata matokeo ya awali kuonyesha kwamba mti huo una uwezo wa kutibu, anasema waliomba ufadhili Costech kwa ajili ya kuangalia magonjwa mbalimbali hasa nyemelezi ambayo yanaathiri mfumo wa ngozi.

Fedha zilipopatikana anasema kwamba waliangalia mti huo kama una uwezo wa kutibu magonjwa ya ngozi.

Anasema walifanya hivyo kwa sababu kati ya masoko ambayo yana vitu vingi vinavyouzika ni vile vinavyosaidia upande wa ngozi maana yake unaanza kwenye sabuni. Kwa kutumia sabuni kinachofuata ni kutumia mafuta, ikitokea bahati mbaya kuna ugonjwa mwingine ambao ni fangasi au vidonda kwenye ngozi.

“Kwa hiyo tukajikita kutafiti upande wa ngozi bahati nzuri kwa huu ufadhili tuliopata tuliangalia kuangalia kama kweli huo mti unaweza kutibu.

“Tukabaini ukizingatia sisi ni watafiti kuna mamlaka zinazotuangalia basi tukaomba ushauri kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na kutupa miongozo inayotakiwa kufuatwa ili mazao yanayopatikana au tunayoyazalisha yanaweza kufikia viwango vinavyokubalika kwa mtumiaji au mlaji katika nchi, ndani ya nchi na nje ya nchi,” anasema.

Anasema alitafiti kujua usalama wake kwa mlaji ndio wakaangalia kwa upande wa vitu vinavyoangaliwa vinavyoweza kuguswa na kunusa, pia kemikali na njia za maikrobailojia hivyo kutambua kitu gani kinatakiwa kufanyika.

Maelezo yake ni kwamba mti huo huwa unakuwa na viini vya aina mbalimbali na viambata vinavyotibu, vipo visivyotibu na vile vitakavyofanya huo mmea utumike kama sabuni au mafuta.

“Tulivyopata hivyo viambata tukaviingiza maabara na kutupa matokeo mazuri hivi tunavyoongea tulijitahidi kutengeneza bidhaa. Kuna bidhaa tulizotengeneza zinazosaidia kwenye mfumo wa ngozi kwa mfano sabuni na losheni,” anasema.

Anasema kwa sasa mapokeo ya matumizi ya miti dawa na bidhaa dawa ni mkubwa, kinachosababisha ziwe kubwa ni hayo wanayoyafanya kuwa kuna njia za kisayansi zinazoboresha hizi bidhaa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Tiba Asili katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Profesa Joseph Otieno anasema kuna aina nyingi za miti maziwa lakini mmojawapo ni ule ujulikanao kama ‘msesewe’ hutumika sana katika kutibu maradhi ya ngozi.

“Inang’arisha ngozi kama mtu ana madoadoa akipaka hiyo madoa yanaisha. Inatibu bakteria,” anasema.

Anazungumzia katika taasisi hiyo ya tiba asili Muhimbili hupokea takribani wagonjwa 200 kwa mwezi.

Anakiri dawa za miti shamba zinasaidia, na hivi sasa hata watu wa mijini wamekuwa wakitumia, tofauti na ilivyokuwa zamani iliaminika kuwa watu wa kijijini waliitumia zaidi kabla ya kutafuta huduma za hospitalini.

“Kama wataalam hatuachi kusema sio kila mti shamba unafaa kutumia. Kikubwa ni kuhakikisha kuwa dawa tunazowapa jamii zetu zinasaidia kisayansi,” anasema.

 

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Watengenezaji Bidhaa Asili Tanzania (Uwabiata), anayefanya shughuli zake eneo la Soko la Kariakoo, Rajab Mbambwa anasema ili uwe mtu wa tiba asili inabidi ukae na watu wa tiba asili kuangalia wanavyofanya ili nawe uelewe.

Anaeleza kuwa uuzaji wa dawa asili alianza siku nyingi akiwa na miaka 25 hadi sasa anakaribia miaka 65.

“Mimi ni mtu wa Ujiji Kigoma pia kule kwetu karibia kila nyumba kuna mtaalam wa tiba asili, hivyo ni rahisi kujifunza kwa urahisi,” anasema.

Serikali kupitia Costech imeweza kutafiti utafiti huo wa miti dawa ambao umezaa matunda chanya kwa jamii katika kutibu magonjwa kwenye ngozi kupitia sabuni na losheni.

 

Habari Zifananazo

Back to top button