Watahiniwa asilimia 66 wafaulu uhasibu

BODI ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), imepitisha matokeo ya 98 ya bodi ambapo watahiniwa 4468 sawa na asilimia 66.6 wamefaulu mitihani yao katika mitihani iliyofanyika Novemba 2023.

Aidha Bodi hiyo imezindua mihtasari mipya pamoja na vitabu vya rejea ambavyo kwa pamoja vitaanza kutumika kuanzia Januari 2024 na mitihani ya kwanza kwa kutumia mihutasari hiyo itafanyika Novemba 2024.

Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, Pius Maneno amesema hayo leo Dar es Salaam wakati akizungumzia maboresho mbalimbali yaliyofanywa na Bodi hiyo yakianza kutumika kuanzia Januari 2024.

Advertisement

Kuhusu matokeo amesema watahiniwa waliosajiliwa walikuwa 7238, na watahiniwa 527 sawa na asilimia 7.3 hawakuweza kufanya mitihani kwa sababu mbalimbali.

Amesema idadi ya watahiniwa waliofanya mitihani ni 6711 sawa na asilimia 92.7, kati ya waliosajiliwa kufanya mitihani watahiniwa 3636 sawana asilimia 50.2 walikuwa wanawake na watahiniwa 3602 sawa na asilimia 49.8 walikuwa wanaume.

Amesema ufaulu huo ni tofauti na matokeo ya mwaka jana ambapo ufaulu ulikuwa asilimia 67.2 na kwamba mwaka uliofuatia 2021 ufaulu ulikuwa asilimia 70.

Kuhusu uzinduzi wa mihutasari amesema Bodi hufanya mapitio ya mitaala yake pamoja na vitabu kila baada ya miaka mitano na maboresho ya mwisho yalifanyika mwaka 2019.

“Bodi inayo mihutasari mitatu ambayo ni mtaala wa cheti ngazi ya awali ambao una masomo manne, mihutasari ya pili ni wa cheti ngazi ya pili ambao pia una masomo manne, mihutasari wa tatu ni ule wa ngazi ya taaluma ambao una masomo kumi na sita, hivyo idadi ya masomo katika mihutasari yote mitatu ni ishirini na nne,” amesema Maneno.

Amesema Bodi ilianza mchakato wa kupitia mitaala yake pamoja na vitabu vya rejea kuanzia Agosti 2022 kazi hiyo ilianza kwa kufanya marekebisho yamitaala na baada zoezi la kupitia vitabu vya rejea lilifanyika.

Hata hivyo amesema kazi ya kurekebisha mihutasari ilianza kwanza kwa kuchukua maoni kutoka kwa wadau mbalimbali ambapo yalichakatwa na kutumika kama nyenzo mojawapo katika zoezi la mapitio.

“Kazi ya kupitia somo moja baada ya jingine ilifanyika ilikuondoa mada zilizokuwa zimepitwa na wakati na kuingiza mada mpya,” amesema Maneno na kuongeza kuwa mada mpya ambazo hazikuwepo kabisa ziliongezwa na masomo mengine yaliboreshwa kwa kuongeza mada za somo nyingine.

Amesema kwa mfano somola uchumi limeongezewa mada za kodi na somo la uhasibu kuongezewa mada za ukaguzi, masomo yote hayo yako kwenye ngazi ya awali ya taaluma.

Maneno amesema watahiniwa wote wa mitihani ya Bodi waliopo na watakaosajiliwa baadae pamoja na walimu kutumia mitaala hiyo pamoja na vitabu vya rejea kwa usahihi ilikuongeza ufaulu katika mitihani ya Bodi.

Kuhusu wahasibu wahitimu walioomba kupanda kuwa wahasibu au wakaguzi wa hesabu amesema Bodi inawajulisha wote walioomba kupanda daraja kuwa wahasibu na wakaguzi wa hesabu kukamilisha maombi yao ifikapo Machi 15,2024.

Amesema maombi ambayo yatakuwa hayajakamilika hadi kufikia muda huo yatakataliwa na muombaji atalazimika kuanza upya muda wake wa mafunzo kwa vitendo kwa miaka mitatu.

Amesema Bodi inasisitiza kuwa wahasibu wahitimu ambao maombi yao yamerudishwa kwao zaidi ya 500 hadi leo(jana) kwa ajili ya kuyafanyia kazi wayafanyie kazi mapema na kuyarudisha Bodi iwezekanavyo.

“Ikumbukwe kuwa maombi yote ya kupanda daraja yanafanyika kwa njia ya mfumo wa kielektroniki uliowekwa na Bodi na hakuna chombo kingine kinachoweza kufanya majukumu hayo ni Bodi na mhitimu mwenyewe hakuna uwakilishi,” amesema Maneno.

1 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *