Wataka bima ya afya itumike huduma za kuhifadhi maiti

WANANCHI mkoani Mwanza wameomba uendelevu wa huduma za bima ya afya kwa maiti pale mwanachama anapofia hospitalini, badala ya uanachama wake kukoma dakika hiyo anapofariki.

Wametoa maoni hayo wakati wa mkutano wa wadau kuhusu muswada wa bima ya afya kwa wote ulioandaliwa na Wizara ya Afya, kwa makundi maalum kama vile viongozi wa dini, wavuvi, wakulima, waendesha pikipiki maarufu kama ‘bodaboda’ pamoja na wajasiriamali, wakiwemo machinga.

Mjumbe wa Halmashauri ya Baraza la Waislamu (Bakwata) Mkoa wa Mwanza, Twaha Utali, ameshauri huduma za kuhifadhi mwili wa mwanachama ziwe sehemu ya bima na zitolewe hadi mwili utakapokabidhiwa kwa ndugu.

“Huduma hizo zihusishe pia dawa inayochomwa maiti kwa ajili ya kuhifadhi mwili, ambayo mara zote imekua ikigharamiwa na wanafamilia,” ameshauri.

Maoni mengine yaliyotolewa ni kadi ya bima kwa wote kugharamia huduma zinazotolewa na waganga wa kienyeji wanaotambuliwa na serikali.

Msemaji  wa Chama Cha Wavuvi Mkoa Mwanza, Sijaona James, amesema wapo wagonjwa ambao matibabu yao yanashindikana hospitalini na kuhamishiwa kwa waganga wa kienyeji, hivyo kadi ya bima kwa wote imhudumie mwanachama hadi eneo hilo.

“Lakini pia kuna umuhimu wa kuondoa ukomo wa idadi ya wanachama kwa kaya, kutoka sita inayopendekeza katika muswada, kwani wenyeji wa Kanda ya Ziwa wanazaliana hadi kufikisha watoto kumi katika familia,” amependekeza.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Prof Abel Makubi, amesema hoja zote zimechukuliwa na zitafanyiwa kazi, lakini akawataka wananchi kuchangamkia fursa hiyo ya bima kwa wote, ambayo moja ya manufaa yake makubwa ni kuwaondoa Watanzania katika umaskini.

Amefafanua kwamba wapo wanaouza mali zao, ikiwemo mashamba na mifugo ili kupata huduma za matibabu na hivyo kurudi kwenye umaskini.

“Sasa dhamira ya bima ya afya kwa wote ni kuwaondoa wananchi kwenye umaskini wa aina hiyo kwa sababu matibabu yanalipiwa kabla ya mtu kuumwa,” amesema.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x