Wataka gongo idhibitiwe inachochea ubakaji

Madaktari waonya unyweshaji watoto pombe

WANAWAKE katika Kata ya Mamire wilayani Babati mkoani Manyara wamesema vitendo vya ubakaji kwenye maeneo yao vimekuwa vikisababishwa na matumizi yaliyokithiri ya pombe kali ya kienyeji aina ya gongo.

Wameeleza hivyo walipokuwa wakijadili masuala mbalimbali na fursa zilizopo kwa wanawake walipokutanishwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP).

Walisema kukithiri kwa pombe hiyo hapo kijijini kumekuwa kukisababisha matukio mengi ya ubakaji kutokana na ulevi uliopitiliza.

Advertisement

Mkazi wa Mamire, Marry Joram alisema: “Gongo ni shida katika eneo letu, tungeomba serikali itusaidie kwenye hili kwa sababu hawa wanaokunywa gongo ndio wabakaji.”

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Anna Mbogo alisema uuzaji wa gongo ni suala mtambuka, kinachotakiwa ni kuwakusanya vijana wanaojihusisha na biashara hizo na kuwaeleza madhara yatokanayo na pombe hiyo kwani vijana wengi wanaotumia pombe hiyo wameharibika na kupoteza uwezo wa kufikiri na nguvu.

“Kuna watu wanaomiliki mitambo hii, matajiri wakubwa ambao ndio wanawatumia vijana hawa wadogo kwa kuwakodisha, tunachotakiwa kufanya ili kukomesha jambo hili ni kuwatafuta hawa matajiri kwa lengo la kutokomeza hiyo mitambo yao ya kutengenezea,” alisema Mbogo.

Mbogo akaeleza kuwa shida ya mkoa huo ni wananchi wake kuwa na tabia ya kuficha mambo kwani usiri huo unapofanyika hata kama ni mtu amelewa lakini watu hawatoi taarifa kwa mamlaka husika ili aweze kuchukuliwa hatua.

Pendo Johnson kutoka Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Babati alisema shida iliyopo kwa wananchi hao ni kutotoa ushirikiano kwa dawati hilo pale wanapoamua kupambana kwa ajili ya kutafuta haki ya mtu ambaye amefanyiwa ukatili, badala yake wamekuwa wakikimbilia kulipana fidia kwa kuchinja dume ama kulipana fedha.

Naye Mratibu wa Mradi wa Wanawake Vijijini kuleta Mabadiliko, ambao upo chini ya TGNP, Catherine Kasimbazi alisema shirika hilo linajenga uwezo wa watu mbalimbali ikiwa ni wanajamii wenyewe na viongozi wa serikali kwenye bajeti ya mrengo wa jinsia ambao wanaamini ni keki ya taifa na inatakiwa kuwafikia wote ikiwemo makundi ya pembezoni.

Alisema mradi huo ambao ulianza mwaka 2021 na unatarajia kuisha 2026, utafanyia kazi maeneo matatu ambayo ni wanawake katika uongozi na ngazi za maamuzi, upingaji na kukabiliana na masuala ya ukatili wa kingono na mila na desturi zenye madhara kandamizi  pamoja na unufaikaji wa wanawake katika uzalishaji wa chakula kibiashara na mabadiliko ya nchi.