Wataka rushwa ya ngono itenganishwe na nyingine
MTANDAO wa Kupinga Rushwa ya Ngono Tanzania, umemwomba Rais Samia Suluhu Hassan na Bunge la Tanzania, kukataa pendekezo la kifungu cha sheria kinachofananisha rushwa ya ngono na nyingine.
Mtandao huo wenye mashirika jumuishi zaidi ya 150, ulitoa ombi hilo Dar es Salaam jana katika tamko la pamoja lilisomwa na Mwenyekiti wa Mfuko wa Udhamini wa Wanawake Tanzania (WFT-T), Profesa Ruth Meena.
“Serikali iko kwenye mchakato wa kubadilisha sheria ya kupambana na rushwa ikiwa ni pamoja na kifungu cha 25 kinachobainisha rushwa ya ngono na rushwa nyingine kwa kuongeza kipengele 25 (ii) ambacho kinafananisha rushwa ya ngono na rushwa nyingine…” alisema Profesa Meena.
Akaongeza: “Kwa mantiki hii, sisi wanamtandao tunaopinga rushwa ya ngono, kwa pamoja tunapinga kitendo cha kuingiza kipengele cha 25 (ii) cha kumhukumu anayedaiwa rushwa ya ngono kwani kufanya hivyo ni kuendelea kuwalinda wenye mamlaka katika ngazi zote kuwanyanyasa, kuwakandamiza na hatimaye kusababisha vifo vya watoto, wanawake na hata vijana wa kiume wa Tanzania.”
Kwa mujibu wa mtandao huo, kifungu hicho kinamaanisha kuwa, mwanamke aliyelazimika kutoa rushwa ya ngono kuokoa maisha ya mtoto, wanafunzi waliofelishwa mitihani kwa kukataa rushwa ya ngono, wanawake walionyimwa leseni ya biashara kwa kukataa rushwa ya ngono na waathirika wengine, watachukuliwa na sheria kuwa ni wakosaji.
Profesa Meena alisema: “Tunaviomba vyombo vyote vinavyohusika na mabadiliko ya sheria hii ikiwa ni pamoja na ofisi ya mwanasheria mkuu, bunge letu tukufu na hatimaye Mheshimiwa Dk Samia Suluhu Hssam, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wasikubali pendekezo la kubadili hiki kifungu pendekezwa cha sheria hii.”
Kwa sasa mtandao huo unaendesha kampeni dhidi ya rushwa ya ngono yenye kaulimbiu isemayo: “Vunja Ukimya; Rushwa ya Ngono Inadhalilisha na Inaua.”
Wakati huohuo: Mtandao huo umeiomba serikali na watendaji katika ngazi zote, kuendelea kuboresha sheria zanazowalinda Watanzania wote; wake kwa waume kwa kuendelea kutumia taarifa za kitafiti zinazotokana na uchunguzi wa taasisi na vyombo vya habari kubainisha mifumo rasmi na isiyo rasmi ili kuboresha haki za wanawake, wasichana na Watanzania kwa ujumla