Wataka sheria ihoji uamuzi wa DPP kufuta kesi

VYAMA vya siasa nchini vimependekeza itungwe sheria ya kuipa mahakama mamlaka ya kuhoji sababu za Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) kufuta kesi na kukamata tena washitakiwa  na  kufanya maamuzi kama mapendekezo yao yana mashiko au la.

Vimesema kwa sasa hakuna mtu anayehoji sababu za DPP kufuta kesi hata baada ya mashahidi kusikilizwa na baadaye watuhumiwa kukamatwa tena na kufunguliwa kesi inayofanana na ya mwanzo hivyo, kuanza upya jambo ambalo linadaiwa ni matumizi mabaya ya madaraka.

Akizungumza baada ya kuwasilisha mapendekezo ya kuboresha Taasisi za Haki Jinai nchini, Mwanasheria wa Chama cha Wananchi (CUF), Mashaka Ngole alisema  DPP amepewa mamlaka chini ya Sheria ya Huduma ya Mashitaka (NPS) kifungu cha 9.

Pia  kifungu cha 91(1) kinampa mamlaka DPP kuondoa kesi mahakamani wakati wowote kabla ya hukumu bila kutoa sababu.

“Mamlaka haya yamewekwa kwa nia njema kwamba zipo kesi ambazo DPP anaona hana ushahidi na namna pekee ni kuiarifu mahakama ni kutokuwa na nia ya kuendelea na kesi, lakini kumekuwa na matumizi mabaya ya mamlaka haya,” amesema Wakili Ngole.

Ameeleza kuwa hivi sasa imekuwa kawaida kwa waendesha mashitaka kudai kuwa DPP hana nia ya kuendelea na mashitaka dhidi ya mashitakiwa na baada ya kuachiwa hukamatwa na polisi na kufunguliwa kesi inayofanana na ya mwanzo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button