WADAU wa elimu mkoani Mwanza wamelalamikia kutokuwepo kwa uwiano sawa wa walimu kati ya halmashauri za mjini na vijini.
Walidai hali hiyo inakwamisha watoto wa vijijini kupata elimu bora, na hivyo kuwa kikwazo kupata maendeleo endelevu ya kielimu kimkoa na kitaifa ikiwemo ufaulu kitaaluma na kimaisha kwa ujumula.
Wadau waliibua hoja hiyo katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kilichofanyika hivi karibuni mkoani hapa.
Ofisa wa Taaluma Takwimu mkoani Mwanza, Jovither Mwombeki alisema Mkoa wa Mwanza una jumula ya walimu wa msingi 12,529 huku Halmashauri ya Mwanza jiji ikiwa na walimu wa msingi 2,329 na Ilemela 1,484 sawa na walimu wa msingi 3,813 kwa ujumla.
Kwa upande wa halmashauri ambayo sehemu zake nyingi ni za vijijini ikiwemo Ukerewe ina walimu wa msingi 1,164 na Kwimba ikiwa na walimu 1,613 sawa na jumla ya walimu 2,777 wa shule za msingi katika halmashauri hizo mbili.
Alisema shule nyingi za vijijini zina walimu wachache kulinganisha na za mjini.
Mbunge wa Jimbo la Sumve lililopo katika Halmashauri ya Nkwimba, Kasalali Mageni naye alisema shule za Sumve vijijini zina walimu wachache, wasiotosheleza idadi ya masomo yanayopaswa kufundishwa.
“Kuna shule zina walimu watatu au watano, hali inayofanya wanafunzi wasipate elimu bora kutokana na kutokusoma baadhi ya masomo au mada ipasavyo,” alisema.
Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa la Charismatic Episcopal Church of Tanzania (CECT), Charles Sekelwa ambaye pia ni mwenyekiti mwenza wa kamati ya amani mkoani Mwanza, alisema kuwa tatizo kubwa ni wale wenye mamlaka ya kugawa walimu kutopanga walimu wa kutosha katika halmashauri za vijijini.
Askofu Sekelwa alisema changamoto kubwa ni uadilifu kwa watu wenye dhamana ya kugawa walimu kupendelea maeneo ya mjini ambapo wengine hushawishiwa na walimu wenyewe ambao wengi hutaka kubaki maeneo ya mjini hata kama ni kwa rushwa.
Kwa upande wake, Shehe Mkuu Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke alisema ili kutatua changamoto hiyo ya walimu wengi kung’ang’ania maeneo ya mjini lazima miundombinu iboreshwe hasa nyumba za kuishi walimu zitakazowafanya wawe na sehemu ya kukaa wawapo shuleni.