Watakaoshinda uchaguzi CCM wapewa neno

WAGOMBEA wa nafasi za uongozi katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliopitishwa na Halmashauri Kuu ya chama hicho (NEC), wamehimizwa kuzingatia uwazi, uwajibikaji na kuheshimu haki za binadamu.

Akizungumza na HabariLEO, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika Idara ya Sayansi ya Siasa, Dk Richard Mbunda alisema uwazi, uwajibikaji na usimamizi wa haki za binadamu ni changamoto kubwa ambazo zitawakabili viongozi wote watakaopita katika uchaguzi huo wa ndani.

Alisema viongozi watakaochaguliwa wanapaswa kuelewa dunia inapoelekea inahitaji mambo matatu makubwa ambayo ni kuwepo kwa mifumo inayohimiza uwajibikaji, uwazi, kutambua, kujali na kuheshimu haki za binadamu.

Dk Mbunda alisema haki za binadamu zimegawanywa katika makundi mengi ikiwemo haki za kisiasa kwamba wasione fahari kwa chama chao kufanya mikutano huku vyama vingine vikizuiwa kufanya hivyo.

Vilevile alisema viongozi watakaochaguliwa wanapaswa kuhakikisha wanatimiza majukumu yao ikiwemo kuisimamia serikali katika kutekeleza kazi zake kama ambavyo wananchi waliwaamini na kukifanya chama hicho kuendelea kutawala nchini.

“Wanapaswa waelewe kuwa huu si wakati wa kukaa kimya hata pale wanapoona mambo hayaendi sawa serikalini ni lazima watambue wajibu wao kwa sababu jukumu la CCM na wawe ni viongozi ambao wana uwezo wa kuisimamia serikali kwa kufahamu mifumo ya utendaji serikalini na uwazi na sio kuwa nyuma nyuma huku wakisubiri upinzani waseme na wao watetee, hapana!” alieleza Dk Mbunda.

Aliongeza kuwa viongozi hao wakitekeleza majukumu yao ya kuisimamia serikali watakifanya chama hicho kuendelea kuwepo madarakani.

Pia alisema chama hicho kimetumia demokrasia ya kupitisha majina mengi katika nafasi moja lengo kutoa uwanja mkubwa kwa wapiga kura kuchagua viongozi sahihi.

Dk Mbunda alisisitiza kuwa endapo chama hakitasimamia kanuni na taratibu za uchaguzi ikiwemo kufuatilia matumizi ya fedha na rushwa, kitakwama.

“Mwaka 2020 chama kilikuwa na namna ya kudhibiti rushwa katika uchaguzi wa ndani kwa kueleza kuwa ingewakata wagombea ambao wamehusishwa na rushwa lakini hawakutekeleza kwani tuliona nguvu za wajumbe,” alifafanua.

Alisema kama itatekeleza kwa vitendo kuondoa wagombea watakaobainika kutumia rushwa ili kupenya kwenye uchaguzi, itabadilisha taswira ya uchaguzi nchini kwani wagombea wangeogopa.

Habari Zifananazo

Back to top button