Watakiwa kubuni usalama mifumo ya mitandao
TUME ya Tehama nchini (ICTC), imesema ni muhimu sana vijana kuwa wataalam pamoja na kufanya bunifu katika maeneo ya usalama wa mifumo ya mitandao ili kuwa na uchumi wa kidigatali wenye kuzalisha kazi kwao na kufanya Tehama ichangie pato la Taifa.
Mkurugenzi Mkuu wa ICTC, Dk Nkundwe Mwasaga amesema hayo leo Dar es Salaam wakati akifunga mafunzo kwa vijana na wanawake wajasiriamali, kuhusu namna ya kujilinda pindi wanapokuwa wakifanya mambo mbalimbali ya mtandaoni.
Mafunzo hayo ya siku tatu yaliandaliwa na kuratibiwa na Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC) kwa udhamini wa Shirika la Kijerumani la Ushirikiano wa Kimataifa ( GIZ).
Dk Nkundwe amesema kimsingi mitandao kwa kawaida inatakiwa iwe na usalama pia kuhakikisha inaaminika kwa mtumiaji wa mwisho, hivyo wajikite kuwa wabunifu katika eneo hilo, jambo litakalosaidia kukua kwa uchimi wa kidigitali na kusaidia kuaminika pia.
“Vijana waoneshe uwezo mkubwa utakaosaidia mifumo kuwa salama, ili watu watakapokuwa wakifanya biashara zao ziweze kuwa salama bila kupoteza vitu vyao na zaidi waweze kuaminika,” amesema Dk Nkundwe.
Amesema mafunzo yaliyotolewa na EABC yanatakiwa kuwa mengi haswa kwa kuwa nchi inajenga uchumi wa kidigitali mkubwa, ambao una nguzo moja ya msingi inayoelezea mifumo iwe salama na iaminike.
Amesema katika kuhakikisha mifumo inakuwa salama serikali imetunga sheria mbalimbali ikiwemo ya ulinzi wa taarifa binafsi za watu, makosa ya kimtandao ni yapi zote hizo kwa pamoja zikiwa na lengo la kuhakikisha usalama wa mifumo ya kimtandao.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa EABC, John Kalisa amewataka vijana kufanya kazi kwa bidii kuwezesha mifumo ya kimtandao inakuwa salama kwa kuwa ni eneo linaloweza kuwainua kwa kuwapa ajira.
Ametolea mfano nchini Uganda kuwa asilimia 38 ya biashara zilizomo zinaendeshwa na vijana hivyo wajikite kufanya kazi kwa bidii kuwa na kampuni kubwa zinazoweza kutengeneza mifumo ya kutoa ulinzi wa mitandao.
Amesema majukwaa ya mafunzo kama hayo kwa vijana ni eneo linalozalisha ubunifu, wakifanya kazi kwa pamoja kwa ajili ya kukuza uchumi wa kidigitali.