Watakiwa kuchangia chakula kwa wanafunzi

KATIKA Kujenga upatikanaji wa elimu bora nchini, jamii imetakiwa kuchangia chakula ili wanafunzi waweze kushiriki vyema katika masomo na kukidhi mahitaji ya elimu nchini.

Akizungumza jijini Dar es Salaam Meneja miradi wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET,) Martha Makala amesema ni wajibu wa jamii kushiriki katika uboreshaji na upatikanaji wa elimu bora nchini Tanzania.

“Serikali ina nafasi na jamii lazima iangalie namna inavyoweza kuchangia katika kuboresha upatikanaji wa elimu bora nchini ikiwemo kuchangia chakula ili wanafunzi washiriki vyema katika masomo na kuongeza ufaulu…

“Hii pia itasaidia kupunguza vishawishi vinavyosbabisha mimba za utotoni kwa baadhi ya wanafunzi kupokea fedha kwa ajili ya chakula,” amesema.

Pia amesema jamii inatakiwa kushirikiana na serikali za mitaa na asasi za kiraia katika kuhakikisha elimu inakidhi mahitaji ya Taifa kwa kuhakikisha rasilimali zinatumika kwa usahihi.

‘’Mradi huo uliofadhiliwa na Asasi ya Foundation for Civil Society (FCS,) umetekelezwa katika Halmashauri 10 Tanzania Bara uliwalenga wadau katika ngazi ya jamii, halmashauri za wilaya, asasi zinazofanya kazi katika eneo husika, watunga sera na wabunge,”amesema.

Kwa upande wake Mshauri wa Masuala ya Elimu na Maendeleo Japhet Makongo akizungumzia matokeo ya mradi huo taarifa za makadirio ya mapato ya fedha za shule na matumizi zimekuwa hazifahamiki vyema kwa jamii na wazazi.

“Wazazi pia hawana taarifa sahihi na hawashirikishwi katika vipaumbele vya shule ikiwa ni pamoja na mpango na mchakato mzima wa mapato na matumizi pamoja na baadhi vijiji na viongozi wa vijiji kutofuata kalenda ya kuitisha mikutano ya kila mwezi ambapo taarifa kuhusu sekta ya elimu zingewakilishwa,” amesema.

Katika kuhakikisha jamii inakuwa sehemu ya kukuza sekta ya elimu makundi mbalimbali ikiwemo walimu, wazazi na viongozi wa dini wameonesha ushiriki wao katika shughuli za kijamii.

Habari Zifananazo

5 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button