Watakiwa kuchukua hatua uwepo wa El Nino

napenda kutoa msisitizo kuwa, katika majadiliano haya, ni vyema kujikita kufanya tathmini na kuainisha athari zinazoweza kujitokeza katika msimu huu na kuchukua hatua stahiki

MKURUGENZI Msaidizi (Operesheni na Uratibu), Idara ya Menejimenti ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera , Bunge na Uratibu), Luteni Kanali Selestine Masalamado, amezitaka sekta kuchukua hatua stahiki kipindi cha uwepo wa hali ya El Nino katika msimu wa mvua za vuli 2023.

Hayo ameyasema wakati wa Mkutano wa 22 wa Wadau wa Utabiri wa msimu wa Mvua za Vuli, ulioandaliwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa kushirikiana na Shirika la Save the Children kwa uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uratibu wa Maafa.

“Kama alivyoeleza Kaimu Mkurugenzi Mkuu, juu ya uwepo wa hali ya El Nino, napenda kutoa msisitizo kuwa, katika majadiliano haya, ni vyema kujikita kufanya tathmini na kuainisha athari zinazoweza kujitokeza katika msimu huu na kuchukua hatua stahiki,” amesema Masalamado.

Advertisement

Ametoa wito kwa wadau kutoka sekta mbalimbali kushirikiana na TMA ili kufanikisha upatikanaji wa taarifa za kisekta.

Pia ameipongeza TMA kwa kuendelea kushirikisha wadau mbalimbali katika shughuli zao za utoaji wa huduma za hali ya hewa, ambazo ni pamoja na utabiri wa misimu ya mvua.

Mkurugenzi Msaidizi wa Operesheni na Uratibu, Idara ya Menejimenti ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Luteni Kanali Selestine Masalamado

Amesema ushirikiano unaofanyika ni mfano wa kuigwa na unafaa kuendelea hasa katika kipindi hiki ambapo nchi yetu na dunia kwa ujumla inakabiliwa na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa  la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC) Dk Ladislaus Chang’a alieleza kuwa ni muhimu  izingatiwe kuwa katika msimu huu wa vuli, 2023 mifumo ya hali ya hewa inaonesha uwepo wa hali ya El Nino,  ambayo ilianza kujitokeza mapema mwezi Juni, 2023 na imeendelea kuimarika.

“Mkutano huu ni muhimu sana kwa wadau wa hali ya hewa kupata fursa ya kujifunza kwa undani na kuongeza uelewa kuhusu matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa katika sekta mbalimbali na hivyo kuendelea kuboresha na kuongeza tija,” amesema.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA Dk. Ladislaus Chang’a .

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Programu kutoka Shirika la Save the Children,  Anatoli Rugaimukamu, amesema kikao hicho kinatoa mwelekeo wa jinsi ya kujipanga kukabiliana na maafa hususani kwa waathirika wakubwa ambao ni watoto.

11 comments

Comments are closed.

/* */