WAKULIMA wameshauriwa kuendesha kilimo mseto cha mchanganyiko wa mazao ya chakula na ufugaji nyuki, kwa uhakika wa mavuno ya kutosha na yaliyo bora.
Wito huo umetolewa leo na wataalamu wa ufugaji nyuki wa Wakala wa Misitu nchini (TFS), wakisema uhakika wa mazao ni kwa sababu nyuki wanasaidia kuchavusha mazao kwa wingi, huku nyuki wakipata chakula cha kutosha kuzalisha asali kutoka katika maua ya mazao hayo.
“Tafiti zinaonesha kwamba nyuki anapotua kwenye mmea kutafuta chakula anafanya uchavushaji mkubwa unaosaidia upatikanaji wa mazao mengi ya shambani,” amesema Mhifadhi wa TFS Wilaya ya Butiama, Hafidhi Said.
Amesema chakula anachopata nyuki kwenye mmea huo anaochavusha kinasaidia uzalishaji mkubwa wa mazao ya nyuki, hasa asali na nta.
Amesema kilimo hicho kinapaswa kufanyika jirani na misitu ya hifadhi, kwani ndiyo maeneo salama kwa mujibu wa taratibu zinazoelekeza nyuki kufugwa kilometa takribani sita kutoka kwenye makazi ya watu, ili kuepusha madhara yanayoweza kusababishwa na nyuki kwa binadamu au mifugo.
Akifafanua zaidi, amesema kilimo mseto kinasaidia uzalishaji wa mazao ya nyuki kuwa mkubwa, kwani kinawapungizia nyuki safari ya kwenda kutafuta chakula mbali.
“Kawaida nyuki husafiri hata kilometa sita kutafuta chakula, hivyo kilimo mseto kitamsogezea chakula karibu na kumpatia muda mwingi wa kufanya uzalishaji katika mzinga,” amesistiza.