Watakiwa kufanya maandalizi kidato cha kwanza
WAZAZI na walezi wenye watoto waliohitimu darasa la saba mwaka huu, wametakiwa kuhakikisha wanafanya maandalizi ya kidato cha kwanza mapema kabla ya mwezi Desemba.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko, alipokuwa akizungumza na Daily News Digital na kusema kuwa mwaka huu ufaulu unaweza kuongezeka kwa kiasi kikubwa.
Amesema Mkoa wa Katavi umepokea kiasi cha Sh Bilioni 2.3 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 119 ya shule za sekondari katika halmashauri tano za mkoa huo.
Amewakumbusha wazazi na walezi moja ya wajibu wao ni kuandaa sare za shule na madaftari.
Katika hatua nyingine, amewataka wahitimu wa darasa la saba, kutojiingiza kwenye mambo yasiyostahili kwa umri wao.
Jumla ya watahiniwa 19,052 mkoani Katavi wamehitimu masomo ya darasa la saba mwaka huu, ambapo kati yao wavulana ni 8,876 sawa na asilimia 47 na wasichana 10,176 sawa na asilimia 53.