Watakiwa kufuata taratibu usajili wa dawa

WADAU wa dawa nchini wametakiwa kufuata sheria na taratibu, ili kukamilisha usajili kwa haraka na kuepuka malalamiko ya kuchelewa kwa usajili wa dawa .

Akizungumza leo  jijini Dar es Salaam katika warsha ya wadau wa dawa kujadili kwa kina changamoto zinazohusiana na usajili wa dawa, Mkurugenzi wa Dawa za Binadamu na Wanyama kutoka Mamlaka ya Dawa na Vifaatiba(TMDA),Yona Mwalwisi amesema wanategemea kupata maoni ya wadau, ili waweze kuboresha huduma.

“Tumekutanisha wadau wa famasi, hospitali ambao ni watumiaji wa dawa tunategemea na kupata maoni ya vifaa tiba pia ni mkutano muhimu kwa mamlaka, kwani tutapokea maoni ambayo yatasaidia kuboresha mifumo yetu ya usajili, uingizaji na usafirishaji wa dawa nje ya nchi,”amesisitiza.

Amesema warsha hiyo ni muhimu pia katika kutoa mrejesho kwa wadau wao kwa sehemu ambazo hawajaenda vizuri, kwani kuna vitu wanatakiwa watekeleze, hivyo mkutano unatoa nafasi kwa pande zote mbili namna ya kuboresha huduma.

“Suala la dawa na vifaa tiba walengwa ni wagonjwa kama mamlaka tunataka kuhakikisha mgonjwa ambaye anatumia bidhaa hizo apate bidhaa bora, salama na fanisi lengo ni kuendelea kumlinda Mtanzania,”alieleza.

Mwalwisi amesema watatumia nafasi hiyo kuwaelimisha sheria na taratibu za dawa ili wawalinde wananchi.

“Kwenye upande wa uingizaji kikubwa ni kuzingatia sheria na taratibu za uingizaji kulingana na vigezo tunavyohitaji,”amesema.

Habari Zifananazo

Back to top button