Watakiwa kuhifadhi historia ya jamii, taifa

WANA Historia nchini wameagizwa kutumia taaluma na utaalamu wao kwa ajili ya kutoa maelezo sahihi kuhusu mchakato wa ujenzi wa taifa na uzalendo katika nchi, ikiwa ni pamoja na kuhifadhi historia ya jamii na taifa kwa usahihi.

Pia kuchochea fikra tunduizi katika masuala ya kitaifa na kimataifa kwa kuzingatia ushahidi halisi wa kihistoria.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM), Dk Siston Masanja amesema hayo katika Mkutano wa Chama cha Historia mkoani Dar es Salaam, alipomwakilisha Kamishna wa Elimu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Lyabwene Mutahabwa.

Amewataka wana historia kutoa tafsiri sahihi kuhusu historia ya Tanzania inayochochea umoja na utambulisho wa taifa.

“Ninapenda kuona Chama cha Historia Tanzania kinachochea mapinduzi katika ufundishaji na ujifunzaji wa somo la Historia, kinaendelea kuchochea ujenzi wa taifa letu, na kukuza moyo wa uzalendo miongoni mwa Watanzania.

“Wizara ya Elmu, Sayansi na Teknolojia itaendelea kushirikiana na Chama cha Historia Tanzania kuwajengea watoto na vijana wa Kitanzania moyo wa kuipenda na kuithamini historia yao, taifa lao na kutumia historia kama mbegu ya kuchochea uzalendo, utaifa, na fikra tunduizi,” amesema.

Amewapongeza kwa kufanya kongamano hilo kipindi ambacho taifa lipo kwenye mapitiao makubwa ya mtaala wa elimu, kwani Wizara ya Elimu kwa kushirikiana na wadau imegusa maeneo mengi katika mfumo wa elimu.

Ametaja mambo yaliyofanyika kuhusiana na somo la historia kwenye maboresho hayo ya mtaala kuwa ni kuondolewa changamoto ya kujirudia kwa maudhui katika ngazi mbalimbali za ufundishaji wa somo la hilo hasa kwa ngazi ya elimu ya sekondari ngazi ya chini na sekondari ngazi ya juu.

“ Pia somo la Historia sasa litajikita zaidi katika kufundisha na kujifunza historia ya Afrika na dunia kwa ujumla wake. Na pia tumeanzisha somo jipya linaloitwa Historia ya Tanzania na Maadili.,” amesema.

Amesema somo hilo jipya litasomwa katika ngazi zote za elimu pia litakuwa ni la lazima kwa kila mtoto katika mfumo wa elimu ya Tanzania.

Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Historia Tanzania, Dk Osward Masebo amewataka watanzania kutambua kuwa historia ni somo nyeti, la kimkakati kwa usalama wa taifa.

“Ni somo lenye wajibu wa kulipa taifa letu nguvu yake ya ndani na nje. Wajibu wake upo katika kutunza na kulinda misingi ya utamaduni wetu, misingi ya historia yetu, misingi ya utaifa wetu, misingi ya uzalendo wetu, misingi ya maadili yetu na misingi ya urithi wetu,” amesema.

Amesema hatima ya ustawi wa taifa inategemea kiwango cha uwekezaji katika usalama wa historia ya taifa , maadili, mitaala ya elimu pamoja na mitaala ya historia.

Habari Zifananazo

Back to top button