Watakiwa kuimarisha mapato, dawa, vifaa tiba

WASIMAMIZI wa vituo vya afya wa halmashauri za wilaya za Mkoa wa Morogoro wametakiwa kuimarisha makusanyo ya mapato, upatikanaji wa dawa na vifaa tiba ili kuhudumia jamii kwa viwango vya ubora unaostahili.

Rai hiyo ilitolewa juzi mjini Morogoro na Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Morogoro (Tawala na Rasilimali Watu), Herman Tesha wakati akifungua mafunzo ya mfumo wa shitiri ya kuwajengea uwezo waganga wakuu wa halmashauri za mkoa huo, wafamasia, maofisa ugavi na maofisa Tehama.

Mafunzo hayo yalilenga kufanya maboresho makubwa katika sekta ya afya ya kuwa na upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa mfumo wa mshitiri kwenye vituo vya afya kwa urahisi.

Tesha aliwataka watalaamu wa afya baada ya mafunzo hayo kwenda kuboresha na kusimamia ukusanyaji wa mapato kwenye vituo vyao kwani fedha hizo ndizo zitatumika kununulia dawa na huduma zingine za afya.

Aliwataka pia wasimamizi wa vituo vya afya kwenda kutoa mafunzo ya kielektroniki kwa watendaji wenzao wa vituo ili kutanua wigo wa mafunzo hayo. Pamoja na hayo aliwataka kudhibiti upotevu wa dawa ndani ya vituo vya afya kwani kwa sasa yapo malalamiko ya wananchi kuhusiana na suala hilo.

Naye Mwezeshaji wa Kitaifa wa Mfumo wa mshitiri, Dk Abdilahi Njopeka alisema lengo la mafunzo hayo ni kutawanya mwongozo wa utekelezaji wa mfumo huo ili kuongeza ufanisi katika upatikanaji wa dawa nchini.

“Tayari Bohari ya Dawa nchini imeandaa mwongozo unaofanana kwa mikoa yote ya Tanzania Bara kwa ajili ya utekelezaji,” alisema. Dk Njopeka alisema mfumo wa usambazaji wa mshitiri umefadhiliwa na Mradi HPSS-Tuimarishe Afya, unaofadhiliwa na Serikali ya Uswisi kupitia Shirika la Maendeleo na Ushirikiano la Uswisi (SDC).

Kwa upande wake Mshauri Mwandamizi wa masuala ya dawa na vifaa tiba kutoka mradi wa HPSS, Fiona Chilunda alisema wataendelea kushirikiana na serikali kuhakikisha kuwa dawa na vifaa tiba vinapatikana kwa asilimia 100.

Alisema mfumo huo umetengenezwa ndani ya mfumo wa serikali na unaendeshwa na watumishi wa serikali na utafanya kazi pale ambapo MSD ikishindwa kutekeleza mahitaji ya vituo vya afya kwa asilimia hizo 100.

“Pale ambapo MSD wanashindwa kutekeleza mahitaji ya vituo kwa asilimia 100 mfumo huu utaingia kwenye kurusu vituo kuagiza dawa kutoka kwa washitiri binafsi ambao wameshasajiliwa na wana mikataba na mikoa husika,” alisema Chilunda.

Washiriki wa mafunzo hayo akiwemo Kaimu Mganga Mkuu Manispaa ya Morogoro, Dk Mariam Bendera alisema mafunzo hayo yatawasaidia jinsi ya kusimamia bidhaa za afya ambazo ni dawa, vifaa tiba na vitenganishi.

Dk Mariam alisema mafunzo hayo yatawajengea uwezo wa namna gani wataweza kupata dawa au vifaa tiba ambavyo havipo kwenye vituo vyao vya afya na kwamba mfumo huo utaboresha usimamizi namna bora yakutumia ujazaji kwa njia ya kielektroniki.

Habari Zifananazo

Back to top button