Watakiwa kujiandaa uwakala mbolea Geita
MKUU wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella ameziagiza halmashauri zote mkoani hapa kujiandaa kuchukua kibali cha uwakala wa kununua na kusambaza mbolea ya ruzuku kwa msimu wa kilimo 2023/24.
Shigella ametoa maelekezo hayo katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC), ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa mbolea ya ruzuku iliyojitokeza mwaka huu.
Ameagiza kila halmashauri inapaswa kuandaa bajeti na mpango kazi na kuufanya mkakati huo kama sehemu ya huduma na siyo biashara, ili kuwasaidia wakulima kupata huduma kwa wakati na kuongeza uzalishaji.
“Kwa msimu unaokuja, kwenye kila halmashauri, kwanza tuhuishe tupate takwimu ambazo zipo sahihi, la pili tung’amue mahitaji ya mbolea kwenye kila kituo na waajiri wetu wawe sehemu ya uwakala.
“La tatu, ofisi ya RAS (Katibu Tawala Mkoa) iwasiliane na wenye viwanda na waingizaji mbolea kutoka nje ya nchi, waje tuzungumze hapa tuone mahitaji yetu, na utaratibu tutakaotumia ili mbolea iletwe mapema.
“Mbolea zikae kwenye maghala yetu (ya halmashauri), tutakapokuwa tunauza, hela tutakayoipata tutawalipa kwa utaratibu tutakaokuwa tumekubaliana,” alisema.
Ameelekeza, halmashauri zichukue hatua ya dharura kuwatambua wananchi wanaoendelea na kilimo hasa mabondeni, ili waweze kusajiliwa na kupatiwa mbolea ya ruzuku kwa msimu huu.