WATUMISHI wameaswa kufanya kazi kwa bidii, ili malengo yaliyowekwa yaweze kufikiwa katika muda uliobaki kufikia mwisho wa mwaka 2022/2023.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni ( BRELA), Godfrey Nyaisa alitoa wito huo kwa watumishi wakati wa hafla ya kuwapongeza watumishi hodari jijini Dar es Salaam.
“Ndugu watumishi, hivi karibuni Wakala imefanikiwa kujijengea heshima na imani kwa Serikali na wananchi kutokana na kutoa huduma bora, kwa haraka na kwa urahisi, kwa kutumia mifumo ya TEHAMA, hivyo kuwezesha kutimiza malengo yake kwa asilimia 100 au zaidi kila mwaka,” alisema.
Amesema ni jambo muhimu kwa Wakala kuendelea kutunza heshima na imani hiyo kwa kufanya kazi kwa bidii na kuwaelekeza wakurugenzi na wakuu wa vitengo kuhakikisha kwamba malengo yote yaliyopangwa yanakamilika.
Akitaja mafanikio hayo alisema hadi kufikia Mei 9,mwaka huu, Wakala imefanikiwa kukusanya kiasi Sh 25,237,269,777 kati ya lengo iliyojiwekea hadi kufikia Juni mwaka huu la kukusanya Sh 28,904,217,240, kiasi hicho cha fedha ni sawa na asilimia 87 ya lengo lililowekwa kwa mwaka.
Kwa maelezo yake mafanikio hayo yanatokana na Wakala kusajili kampuni 12,398 kati ya 13,100 sawa na asilimia 95, majina ya biashara 23,075 kati ya 25,000 sawa na asilimia 92, Hataza 53 kati 35 sawa na asilimia 151, kutoa Hataza 16 kati ya 35, sawa na asilimia 46, maombi ya Hataza yaliyowasilishwa kupitia ARIPO ni 212 kati ya 650 sawa na asilimia 33.
Vilevile alama za biashara na huduma 3,272 kati ya 4,120 sawa na asilimia 79, kutoa leseni za viwanda 160 kati ya 200 sawa na asilimia 80, kutoa vyeti vya usajili wa viwanda 35 kati ya 44 sawa na asimia 80, kutoa leseni za biashara 13,327 kati ya 13,750 sawa na asilimia 97.