KAGERA; Baadhi ya wananchi wa Kata ya Chanika wilayani Karagwe, mkoani Kagera wameiomba serikali kuwaondoa watu waliovamia vyanzo vya maji na kuanzisha shughuli za kibidamu, hali inayochangia baadhi ya miradi ya maji kuharibika.
Kauli hiyo imetolewa na wananchi katika maeneo mbalimbali wakati Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya na Kamati ya Siasa ya Wilaya zilipokutembelea kukagua mradi wa maji wa chanika.
Akizungumza mjini hapa, Murshid Abudul mkazi wa Chanika amesema endapo hatua za haraka hazitachukuliwa kuwaondoa wananchi wanaofanya shughuli za ujenzi kilimo na mifugo, huenda adha ya maji Karagwe ambayo imevitesa vizazi ikarejea.
Amsema serikali imetumia nguvu kubwa kuwaondoa wananchi katika wimbi la mateso, huku wananchi wakipambana kujirudisha katika wimbi hilo pale wanapoharibu vyanzo vya maji.
Mwenyekiti wa chama Cha Mapinduzi wilaya hiyo, Paschale Rwamugata ameonya wanaanchi wanaoharibu vyanzo vya maji na kuwataka kuheshimu sheria zinavyotaka.
“Naomba mlinde vyanzo vya maji kama mboni yenu, Chama Cha mapinduzi hakitamvumilia mtu anayeharibu vyanzo vya maji, hivyo naomba msitishe shughuli zenu mara moja katika vyanzo vya maji, “amesema Rwamugata.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Karagwe, Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Rasul Shandala, amesema tayari Kamati ya Ulinzi na Usalama, imefanya ziara ya kutoa elimu juu ya athari za uvamizi wa vyanzo vya maji, hivyo wananchi wanaoendelea kuvamia vyanzo vya maji wataondolewa.
“Niendelee kuwaagiza wananchi kutoka mara moja katika vyanzo vya maji na kusogea mbali, ,kupanda miti rafiki karibu na vyanzo vya maji, vinginevyo tutawaondoa kwa lazima, “amesema Shandala.
Meneja wa RUWASA Wilaya ya Karagwe, Cassian Wittike amesema kuwa mradi wa maji wa Chanika_Runyaga _Ruzinga unatekelezwa kwa gharama ya Sh Bilioni 4.2 na kwa sasa umefikia asimilia 75.
Amesema mradi huo unatarajia kukamilika Januari mwaka 2024 na utanufaisha wananchi wapatao 12,689 na kuwaondolea adha ya kutembea zaidi ya kilometa 8 kufuata huduma ya maji.
Comments are closed.