Watakiwa kuongeza ubunifu kuzifikia fursa

SERIKALI imewataka wajasiriamali wa bidhaa nchini kuelekeza nguvu zao katika ubunifu wa kidigitali ili kuweza kuzifikia fursa mbalimbali zenye kuongeza wigo wa masoko ndani na nje ya nchi.

Katibu Mkuu,Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, Dk Zainab Chaula amesema hayo leo  Dar es Salaam katika mkutano wa kwanza wa taasisi ya GS1 inayohusika kutambulisha bidhaa  zinazozalishwa nchini na kuziwekea nembo.

Akizungumza Dk Chaula amesema zipo fursa mbalimbali zenye kuinua wajasiriamali kiuchumi, ambazo hazijafikiwa kwa kiwango kikubwa licha ya kuwepo kwa tatizo la ajira nchini.

“Tuna janga kubwa la ukosefu wa ajira,watu wamesoma, lakini kutwa wanazunguka katika ofisi wakiwa na vyeti, ipo haja ya kupambana akili na kuingia kwenye  ujasiriamali, lakini pia tujikite kidigitali na kuweza kuwafikia masoko mbalimbali,” amesema Dk Chaula.

Amesema wizara yake ina kitengo cha kutoa mikopo kwa wanawake bila riba, hivyo ni vyema kutumia fursa hiyo katika kupambana pia na changamoto ya mitaji kwa wazalishaji.

Amesema serikali ipo tayari kwa ajili ya kuweka mifumo mizuri pamoja na mazingira bora ya wafanyabiashara, hivyo hakuna haja ya kuwepo wanaolalamika bali ni kuamka na kutumia kile kilichopo.

Amesema GS1 ni sehemu ya tiba ya kupunguza mawazo kwa wajasiriamali namna ya kupata soko na kupeleka bidhaa, hivyo ni muhimu wakajisajiliili kupata manufaa.

Amewapongeza wastaafu wote wa serikalini ambao wanaendeleza yale yanayosimamiwa na serikali katika kukuza maendeleo na kwamba ni muhimu kutangaza nembo ya bidhaa za Tanzania 620 yenye kukuza biashara kwa walio wengi kununua bidhaa zinazozalishwa nchini.

Habari Zifananazo

Back to top button