WAKUU wa Mikoa wametakiwa kuhamasisha upandaji miti 1,500,000 ya matunda katika mikoa yao.
Maelekezo hayo yametolewa na Rais Samia Suluhu leo Novemba Mosi, 2022 jijini Dar es Salaam, akizindua mjadala wa kitaifa kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Akitoa maelekezo hayo amesema, tunajidanganya kupanda miti ambayo inaishia kukatwa, ni sawa na kununua nguo kwa bei rahisi, ni kama uwe na laki tatu useme nikienda maduka mengine nitanunua nguo sita bila kujali ubora, unanunua nguo muda mfupi inachanika na kupauka.
“Vivyo hivyo katika upandaji miti, pandeni miti ya matunda, maana mpaka ikatwe kuwe na sababu ya msingi, kama hakuna sababu ya msingi haitakatwa, naagiza wakuu wa mikoa wote kila Mkoa upande 1,500,000 ya matunda, ” amesema na kuongeza;
“Iringa, Njombe pandeni maparachichi, Lindi na Mtwara pandeni mikorosho, pandeni miti ambayo itawaletea manufaa.
“Miti asili badala ya kuikata itumieni kuzalisha asali, taifa gesi wameshajitokeza wanatoa Sh milioni 300 kusapoti jambo hili, kila mwaka ni jambo kubwa, na wengine jitokezeni kuchangia katika mfuko huu, hii itapunguza ukataji miti hovyo na kuongeza matumizi sahihi ya nishati safi ya kupikia,” amesema.
Takwimu zinaonyesha kuwa kaya zinazopikia kwa kutumia mitungi ya gesi ni asilimia 5, umeme asilimia 3 na nishati nyingine safi asilimia 2.2.
“Hii inaonesha bado kuna kazi ya kuhamasisha matumizi ya nishati iliyo safi na salama. Tunapaswa kuwa na mkakati madhubuti wa kisera na kibajeti pamoja na kuweka mazingira wezeshi katika kutatua changamoto za upatikanaji wa nishati safi.
“Kwenye hili serikali peke yetu hatuwezi, tunapaswa kwenda sambamba na sekta binafsi, nashukuru baadhi yao wakiwemo taifa gesi, wameanza kujitokeza tunakwenda nao sambamba, lakini si kisera kwa sababu ni fursa ya biashara hivyo kuna haja ya kuwa na sera inayoshughulikia suala hili, na wengine mjitokeze,” amesema Rais Samia.