WANANCHI hususani wanawake wametakiwa kupata elimu ya fedha kabla ya kukimbilia kukopa na kuishia kupata matatizo mbali mbali kutokana na madeni.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi kiuchumi (NEEC), Beng’i Issa ameyasema hayo leo Februari 15, 2023 na kudai kuwa sekta ya fedha imekuwa ngumu, watu wanataka kujikwamua kiuchumi lakini hawana elimu.
Amesema mwaka jana kupitia mifuko ya uwezeshaji kiuchumi nchini, imetoa mikopo ya Sh trilioni 5.6 kwa watanzania milioni 9.8 kati yao wanawake ni asilimia 53
Hata hivyo, amesema elimu ya fedha na biashara bado ni kikwazo kikubwa kwa wananchi kwani wengi wanashindwa kujikwamua kiuchumi licha ya kukopa fedha lakini namna ya kuzitumia hawajui na kujikuta wakiingia katika mzigo wa madeni yasiyokuwa na tija.
Amesema wanawake wengi wamekuwa wakikopa fedha katika taasisi za kifedha ambazo zimekuwa zikichangia kwa kiasi kikubwa kuwafilisi.
Kuna taasisi nyingi zimeanzishwa nyingine hazina leseni, watu wanaenda wanakopa, ukikopa hasubui jioni unaanza kulipa rejesho au kesho, wakina mama wengi wanakimbilia hii mikopo matokeo yake wanaanza kupata shida.”Amesema Beng’i
Amesema, kinachofanyika baada ya kushindwa kulipa mkopo ni kuchukuliwa vitu vya ndani ikiwemo Kitanda, TV, Friji na vitu vingine vya ndani.
“Serikali iliona hili tatizo hasa vikoba vilipoanza mwaka 2000 na vilianza kupitia asasi za kiraia, watu wakawa wanajifanyia bila kuwa na sheria yoyote.
“Kwa sasa hiyo sheria imeanzishwa ya huduma ndogo za fedha, lakini bado tatizo ni kubwa na tatizo sisi tunalifahamu, ni elimu ya fedha inatakiwa kwa wanawake.”Amesema
Amesema, kwa sababu watu wengi sana wanataka kujikwamua kiuchumi, wanafikiri kujikwamua kiuchumi ni kwenda kuchukua hela .
“ Kuchukua pesa iwe ni kitu cha mwisho katika uwezeshaji, sisi tunasema kabisa unaweza kufanikiwa kufanya jambo lolote lile mradi una utashi, na ukafanikiwa kwa hela yako ndogo ambayo umeweka wewe mwenyewe.
“ Napenda kuchukua fursa hii kuwambia wananchi tusikilimbilie mikopo kama hatuna uhakika wa tunachotaka kufanya kwa sababu mikopo inaweza kuwa mzigo, unaweza kuwa na matatizo yako ukajiongezea matatizo kwa kwenda kuchukua mikopo.”Amesisitiza
Aidha, amesema mikopo inawafanya watu wengi wavuke kibiashara yaani wapige hatua lakini uwe na uhakika wa kile unachokwenda kukifanya, uwe na nidhamu ya huo mkopo.
“Usichukue mkopo ukaenda kulipa ada ya shule utaurudishaje? Ukichukua mkopo ukaenda kununua bati kujenga nyumba, utarudishaje?”Amehoji na kuongeza “chukua mkopo ukafanye shughuli ya kiuchumi ambayo inakuingizia faida ili ukalipe ule mkopo.”Amesema