Watakiwa kupata mafunzo ubora wa bidhaa
KATIBU Tawala Mkoa wa Arusha, Missaile Mussa amewataka wakurugenzi wa Halmshauri mkoani Arusha kubaini makundi au vikundi yanayojihusisha na uzalishaji wa bidhaa zao, ili kupata mafunzo kutoka Tume ya Ushindani (FCC), kwa lengo la kuongeza tija kwa bidhaa na viwango kwenye ushindani wa soko.
Rai hiyo imetolewa leo jijini Arusha na Katibu Tawala, Mussa wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya uhamasishaji wa masuala ya ushindani na udhibiti wa bidhaa bandia kwa wazalishaji na wamiliki wa viwanda Kanda ya Kaskazini.
Amesema endapo vikundi vinavyopewa mikopo na halmashauri vikipata mafunzo ya udhibiti wa ushindani wa kibiashara, vitawezesha bidhaa zao kuingia katika masoko kutokana na ubora.
Naye Mkuu wa FCC Kanda ya Kaskazini, Nonge Juma amesema mafunzo hayo kwa wafanyabiashara wa viwanda vidogo vya kati na vikubwa yana lengo la kuwezesha kuleta tija katika ushindani wa biashara wanazozalisha, ikiwemo kudhibiti bidhaa bandia zisizizosajiliwa na kuleta athari kiuchumi.