Watakiwa kusajili maeneo wapate hati

DAR ES SALAAM; SERIKALI imewataka wananchi hasa wafanyabiashara wenye maeneo ambayo hayana hatimiliki kusajili maeneo yao, ili waweze kupata hati watakazozitumia kuomba mikopo kwenye taasisi za fedha, hivyo kuendeleza biashara zao.

Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mobhare  Matinyi wakati wa uzinduzi wa kliniki ya ardhi kupitia mradi wa uboreshaji usalama wa milki ardhi uliopo chini ya Benki ya Dunia sanjari na utoaji hati, ambapo amesema hata miradı yote inayotekelezwa na serikali nchini ikiwemo ya umeme, mafuta na gesi lazıma iwe na hatimiliki ya ardhi.

Kamishina wa Ardhi Mkoa wa Dar es Salaam, Rehema  Mwinuka amesema Serikali ina nia ya dhati ya kutatua kero za ardhi kwa wananchi kwa kuja na miradi mbalimbal, ikiwemo wa uboreshaji usalama wa milki ardhi, huku akiwaomba wananchi wenye mashauri mbalimbali ya ardhi mahakamani kuyawasilisha kwenye mradi huo.

Kaimu Mkurugenzi Manispaa ya Temeke, Veronica  Malangwa ameeleza kwamba shughuli hiyo ya utoaji hati litapita katika mitaa mitano ya halmashauri ya Temeke na watatoa hati 3244, ikiwa ni hatua ya kusaidia kupunguza kero za wananchi na kuboresha milki zao.

Mwakilishi kutoka Benki ya Dunia, ambao ndiyo wafadhili wa mradi huo Aisha Masanja ameipongeza serikali kwa kuwezesha kupatikana kwa miradi hiyo, ambayo ni chachu ya maendeleo ya taifa na kwamba mradi umefadhiliwa kwa jumla ya Sh bilioni 345 na utafanyika katika halmashauri zote za Mkoa wa Dar es Salaam.

Habari Zifananazo

Back to top button