Watakiwa kusimamia miradi ya serikali

WAHITIMU wa mafunzo ya uwajibikaji Sekta ya Elimu Msingi (AAI) wa wajumbe wa kamati za Ufuatiliaji Matumizi ya Rasilimali za Umma (PETS) wametakiwa kutumia elimu waliyoipata kusaidia vijiji vyao kusimamia miradi ya Serikali.

Wito huo umetolewa leo na msajili msaidizi wa mashirika yasiyo ya kiserikali (TDC) wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Halima Kitumba wakati akifunga mafunzo ya siku tano yaliyotolewa na taasisi isiyo ya kiserikali ‘Usevya Development Society’ (UDESO) kwa wajumbe wa kamati hiyo kutoka katika vijiji vya Kasekese na Lugonesi vilivyopo katika halmashauri hiyo Katavi.

“Natumai mmeiva na mtaenda kufanya yale mliyofundishwa hapa, nyie ni vijiji vya mfano ambao mmepata mafunzo haya, mkawafundishe wenzenu ili kama wananchi tukatambue wajibu wetu” amesema Halima.

Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Evance Mvamila kutoka Arusha ametaja moja ya mada walizofundisha kuwa ni utawala bora, dhana ya ugatuzi wa madaraka kwenda serikali za mitaa ulikusudia nini, mada kuhusu bajeti sambamba na dhana ya ‘PETS’ kama mfumo na muongozo ambao umetolewa na TAMISEMI ambao umeelekeza namna timu hizo zinaweza kufuatilia rasilimali zao ngazi ya kijiji.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya UDESO, Eden Wayimba ameishukuru Serikali ya Tanganyika kwa kukubali mradi utekelezwe ndani ya halmashauri hiyo pamoja na Taasisi ya ‘WAJIBU Institute’ kwa kufadhili mradi huo.

Amewahimiza wahitimu kwenda kuyafanyia kazi mafunzo hayo kwa kukusanya taarifa na kutuma ripoti ya utekelezaji wa miradi ndani ya maeneo yao.

Habari Zifananazo

Back to top button