Watakiwa kusimamisha ujenzi Tunguu

Watakiwa kusimamisha ujenzi Tunguu

WAZIRI wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Zanzibar, Rahma Kassim Ali, amewataka wote walivamia eneo la Serikali, liliopo Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja na kujenga kinyume cha sheria na utaratibu, kusimamisha ujenzi huo mpaka serikali itakapotoa uamuzi wake.

Ametoa agizo hilo wakati wa ziara yake katika eneo hilo  ikiwa ni utaratibu aliojiwekea wa kutembelea maeneo ya serikali, ambayo imegundulika kuna baadhi ya wananchi huvamia na kujenga bila ya kuwa na kibali rasmi cha ujenzi.

Amesema kuna baadhi ya wananchi wanapoona maeneo ya wazi huyavamia na kuanza ujenzi, bila ya kutambua kuwa maeneo hayo ni ya serikali, hivyo amewataka wote waliovamia eneo hilo kusimamisha mara moja ujenzi huo, atakayekiuka agizo hilo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Advertisement

“Tumegundua kuna baadhi ya maeneo ya serikali, ambapo mengine yapo wazi baadhi ya wanachi huyavamia na kufanya ujenzi kwa ajili ya kuweka makaazi, kitendo ambacho ni kinyume na utaratibu, hivyo tumewataka wananchi kusitisha mara moja ujenzi katika eneo la Tunguu.

“Ili kuepusha migogoro ya ardhi nchini ambayo mengine husababishwa na uvamizi wa maeneo kinyume na utaratibu, niwamombe wananchi wanapotaka kufanya ujenzi kufika katika taasisi husika kwa lengo la kupatiwa utaratibu mzuri wa kisheria,” amesema.

Mkuu wa Mkoa Kusini Unguja, Rashid Hadid Rashid amesema kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, watahakikisha wanayasimamia  ipasavyo maeneo yote ambayo baadhi ya wananchi wameyavamia na kufanya ujenzi usio rasmi, ili wasiendelee na ujenzi huo kwa maslahi ya taifa na wananchi wake.

/* */