Watakiwa kutatua changamoto ya maji Muheza

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga, kimezitaka taasisi za Ruwasa, TANESCO pamoja na Tanga Uwasa kuja na suluhisho la muda mfupi kumaliza changamoto ya uhaba wa maji Wilaya ya Muheza wakati wakisubiri kipindi cha mvua.

Agizo hilo limetolewa na Katibu wa CCM Mkoa Tanga, Suleiman Mzee Suleiman, wakati alipotembelea Wilaya ya Muheza, baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi wa wilaya hiyo, ambao kwa sasa wanapitia kipindi kigumu cha ukosefu wa huduma ya maji kwa kipindi kirefu sasa.

Amesema kuwa wakati huu wa kiangazi kutafutwe ufumbuzi wa kuhakikisha wananchi wa Muheza wanapata maji angalau kwa mgao, wakati wakisubiri mvua ziweze kurejesha maji katika vyanzo.

“Ile timu ya wataalamu ikutane tena, iliyohusisha watu wa Tanga Uwasa, Ruwasa pamoja na watu wa Tanesco wakae kwa siku tano watushauri nini kifanyike kama lipo jambo la kufanya la dharura basi lifanyike ili kuweza kutatua kadhia ya maji kwa wakazi wa Muheza, “amesema Katibu Mzee.

Pia Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Juma Irando alisema shughuli za kibinadamu zimechangia kusababisha tatizo la uhaba wa maji katika Wilaya ya Muheza, akitolea mfano mto Magoroto, ambao hivi sasa umekauka.

Naye Meneja wa Maji Kanda Muheza kutoka Tanga Uwasa, Ramadhani Nyambuka, alisema changamoto ya ukosefu wa maji katika wilaya hiyo inatokana na umeme mdogo, ambao unashindwa kuendesha mitambo ya maji

Habari Zifananazo

Back to top button