WATAALAMU na watafiti wa bioteknolojia nchini, wametakiwa kutoa ushauri wa kisayansi wenye tija kwa serikali.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Dk Seleman Jafo, amesema hayo wakati akizindua Mkutano Mkuu wa Chama cha Bioteknolojia Tanzania (BST) jijini Dar es Salaam.
Jafo amesema katika ulimwengu wa sayansi na teknolojia nchini Tanzania kumekuwepo na mgongano mkubwa wa mawazo, watu wamekuwa na hofu, inawezekana ni hofu ya kisayansi, kutokujua faida zake au ya kibiashara.
Amesema ili kuondoa hofu hiyo, wataalam na watafiti wanapaswa kuelimisha jamii kuhusiana na teknolojia hizo ikiwemo ya uhandisi jeni (GMO).
” Watafiti na wasomi tukikamilisha majawabu ya teknolojia zilizopo na tukaweka wazi matokeo, Watanzania wataelewa,” alisema na kuongeza kuwa wataalamu washughulikie mambo ya kitafiti na kitaalam nchi isonge mbele.
Awali Mwenyekiti wa BST, Profesa Peter Msolla amesema pamoja na nchi kuwa na sera zinazohimiza matumizi salama na endelevu ya bioteknolojia ya kisasa, na kuwa na mfumo thabiti wa usimamizi, utafiti wa kutumia teknolojia ya GMO katika sekta ya kilimo umesitishwa kutokana na maelekezo ya wizara husika.
“Tunaishauri serikali kuangalia upya maamuzi hayo kwa sababu bila kufanya utafiti hatuwezi kupata majibu ya maswali yanayoulizwa na wadau mbalimbali kuhusu faida na hasara za bioteknolojia ya kisasa,” amesema.