WADAU wa habari wameaswa kutumia kalamu zao kubadilisha mitazamo kwenye vyombo vya siasa, ili waweze kuongeza nafasi za wanawake viongozi ambao wana sifa za kuongoza katika ngazi zote za jamii.
Wadau wa habari wa masuala ya jinsia na uongozi wamesema hayo katika kongamano la maadhimisho ya miaka 30 ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani yaliyofanyika mjini Unguja
Wamesema ili kubadilisha mitazamo hiyo ni muhimu waandishi wa habari wafahamu matumizi sahihi ya TEHAMA, ambayo kwa sasa ni kipaumbele katika maendeleo.
“Tukaanze kudesign miradi iliyokuwa salama ambayo itawajengea uwezo wanawake waweze kutumia digital salama, ili waweze kufanya uongozi wao, kwa uongozi sisi hatuwezi kutofautiana na watu wengine ila tunawachochea wanawake wawe wajasiri katika kuongoza,wawe na fikra chanya katika kutatua changamoto katika jamii, hivyo vyote wavifanye wakiwa na intaneti,” alisema mwakilishi wa Shirika la Policy, Navina Mtabazi.
Akichangia suala hilo la uongozi, Katibu Tawala Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, Rahel Mhando amesema suala la uongozi linahitaji uwe na taarifa na maarifa sahihi ambayo yataweza kukujenga na kukuongoza katika shughuli za uongozi
“Kuna mabadiliko mengi ya teknolojia , kuna mabadiliko ya sheria kuna mabadiliko ya sera, kuna miongozo na taratibu kadha wa kadha kuligama ma teknolojia zilizopo kulingana na maisha yanavyoenda duniani tunaadopt vitu vingine kwa hiyo lazima uwe na maarifa,” alisema Mhando.
Kwa upande wake mwandishi wa habari na Mtangazaji kutoka Shirika la Utangazaji Zanzibar ZBC, Kauthar Isaack, amesema kuna utamaduni uliojengeka kwa wanawake wengi nchini kuogopa kushindana katika masuala ya kugombea uongozi.
“Kwanza kuna wanawake ambao wao tayari wanaona kwamba kuna mila na desturi malezi na makuzi yaliyotukuza tamaduni zetu kweli anaweza kuwa,” alisema Kauthar
Naye mwandishi wa habari na mtanagzaji mkongwe kutoka kituo cha utangazaji cha Channel Ten, Easther Zelamula aliwashauri waandishi wa habari wanawake wasikate tamaa pale wanapokumbana na vikwazo kazini
“Kwanza ni lazima ujitambue ujithamini self confidence, yaani ujiamini wewe mwenyewe kwani wewe ni nani na kwa nini upo hapo nahata katika utekelezaji wa majukumu yako ni lazima ufanye kwa ufasaha bila kujali maneno ya watu, bila ya kujali pingamizi ya aina yoyote, ili mradi unajielewa na unasimama katika mstari na unajua unachokifanya, basi utakuwa kiongozi mzuri,” alisema Easther.
Katika kongamano hilo wajumbe wamekubaliana kwamba waandishi wa habari wawe ni wabeba maono kufanikisha lengo la ongezeko la viongozi wanawake nchini.