Watakiwa kutunga sheria ndogo kwa kuzingatia katiba, uhalisia

MAMLAKA zilizokasimiwa kutunga sheria ndogo na kanuni zimetakiwa kutunga kwa kuzingatia katiba na uhalisia wa maisha ya wananchi.

Rai hiyo imetolewa Jumatano bungeni Dodoma wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo ikiwasilisha taarifa kuhusu uchambuzi wa sheria ndogo iliyowasilishwa bungeni katika mkutano wa sita na mkutano wa saba pamoja na uchambuzi wa taarifa za utekelezaji wa maazimio ya bunge kuhusu sheria ndogo zilizowasilishwa kwenye mkutano wa tatu na mkutano wa nne wa bunge.

Mwanasheria Mkuu, Dk Jaji Elieza Feleshi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama wakati wa kuhitimisha hoja hiyo kwa nyakati tofauti walizitaka mamlaka hizo zinapotunga sheria na kanuni baada ya kukasimiwa kuzingatia Katiba ya nchi na maisha halisi ya Watanzania na kuondoa migogoro ya kisheria.

Advertisement

Jenista akichangia hoja wakati wa hitimisho hilo alisema wamepokea taarifa na maelekezo ya kamati kuhusiana na sheria hizo ndogo na kanuni kukinzana na sheria mama lakini pia michango ya wabunge imedhihirisha sheria hizo zimekuwa zikisababisha migogoro kwani haziendani na maisha halisi ya Watanzania.

“Nitoe wito kwa mamlaka zilizokasimiwa kutunga sheria ndogo kupunguza dosari hizi kwa kutunga sheria na kanuni zinazozingatia Katiba na kuepuka sheria zinazokiuka haki za msingi za wananchi,” alisema.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Jaji Elieza Feleshi alisema kuna dosari 40,000 katika sheria ndogo zinazoendelea kufanyiwa marekebisho na zinaendelea kuchukuliwa hatua mbalimbali.

“Tusisubiri ugonjwa ukomae, kama kuna dosari zinabainika mapema ziletwe katika ofisi ya mwanasheria mkuu ili ziweze kufanyiwa kazi haraka,” alisema.

Awali Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk Jasson Rweikiza alisema baada ya uchambuzi wa sheria hizo ndogo walibaini kuna maudhui ya sheria ndogo saba zinazokinzana na masharti ya sheria mama na sheria nyingine za nchi.

Alitoa mfano wa sheria ndogo hizo ni kuwa ni pamoja na ya The Electricity (Electrical Installation Services) Rules, 2022 (TS. Na.113/4, Machi 2022) ambayo imetungwa chini ya Sheria ya The Electricity Act (Sura 131) na kuwa kwa tafsiri ya kawaida, leseni ni idhini maalumu kutoka kwenye mamlaka inayohusika ili kufanya shughuli au kazi mahususi, hivyo shughuli au kazi yoyote nje ya idhini hiyo au bila ya idhini hiyo inahesabika kufanyika bila leseni.

Alisema Kanuni ya 4 imeweka wajibu wa kuomba na kupata leseni kwa ajili ya kufanya shughuli ya kuunganisha umeme na kwa msingi huo, kufanya shughuli ya kuunganisha umeme pasipokuwa na leseni kosa linalostahili adhabu kwa mujibu wa kanuni hizi, lakini Kanuni zimeweka adhabu mbili tofauti kwa makosa ya kuunganisha umeme pasipo na leseni.

Dk Rwekiza alisema adhabu ya kwanza imetajwa katika Kanuni ya 4(2) ni faini isiyozidi Sh milioni moja au kifungo cha muda usiozidi miaka mitano au vyote na adhabu ya pili imewekwa na Kanuni ya 21(1) ambayo ni faini ya Sh 200,000 kwa mwenye leseni anayefanya kazi ya kuunganisha umeme iliyo nje ya wigo wa leseni yake.

Kwa mujibu wa Dk Rweikiza, adhabu zilizowekwa na Kanuni ya 4(2) na 21(1) zinakinzana na adhabu iliyowekwa na Kifungu cha 8(5) cha sheria mama ambacho kifungu hicho kinatamka adhabu ya Sh milioni 10 au kifungo kisichozidi miaka mitano au adhabu zote mbili kwa pamoja kwa kosa la kuunganisha umeme bila leseni.

 

 

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *