BENKI Kuu ya Tanzania (BoT), imewataka wananchi kutunza fedha vizuri, ili zisichakae haraka na kuisababishia gharama serikali kuchapisha zingine.
Hayo yamesemwa leo na Meneja Msaidizi Sarafu kutoka BoT, Nolasco Maluli, wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa utambuzi wa alama za usalama na utunzaji fedha walemavu wa kusikia (viziwi) Mkoa wa Dodoma.
Alisema kuwa utengenezaji wa noti na sarafu unaigharimu serikali fedha nyingi, hivyo utunzaji mzuri ni jambo lenye tija.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo Meneja Msaidizi Sarafu (AMS), tawi la BOT Dodoma, Nolasco Maluli alisema kuwa lengo ni kuwafanya wanachama hao kuzitambua alama za usalama za noti, ili kuepuka kuibiwa kwa kupewa fedha bandia.
Katika mafunzo hayo CHAVITA Dodoma wamefundishwa kutambua alama kwa macho, kwa mguso wa mikono pamoja na kutumia vifaa maalum kama mwanga wa taa maalum.
Alisema kuwa ili kuzitambua noti halisi kuna alama muhimu nne ambazo wanapaswa kuzifahamu ikiwemo picha ya hayati Mwalimu Nyerere, utepe na alama nyingine.
Katika mafunzo hayo pia CHAVITA walifundishwa namna nzuri ya kutunza fedha ili zisichakae kwa haraka.
Atufigwege Mwakabalula Ofisa wa Benki Kuu alisema kuwa kwa kawaida fedha za Tanzania zinatengenezwa kwa pamba, hivyo haifai kuwekwa katika eneo lenye unyevunyevu.
Alisema kuwa fedha zinapochakaa serikali inaingia gharama kubwa kutengeneza fedha nyingine mpya, jambo linaloathiri utekelezaji wa miradi mingine ya kimkakati.
“Tusipozitunza vizuri hizi fedha tunaipa serikali gharama ya kuchapisha fedha nyingine mpya kila wakati, na fedha hizi zinachapishwa kwa fedha za kigeni hivyo tunaweza kuona ni gharama kiasi gani serikali inatumia,” alisema.
Aliongeza kuwa ni vyema fedha zikatunzwa katika vibebeo maalum kama vile pochi na kuwataka kuacha kuzikunja na kuzihifadhi ardhini.