Watakiwa kutunza miradi ya TASAF
GEITA; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,George Simbachawene amewasihi wananchi kuthamini na kutunza miradi inayotekelezwa na serikali ikiwemo ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika maeneo yao, kwani ina lengo la kuondoa umaskini katika jamii.
Simbachawene amesema hayo alipokuwa akizungumza kwa nyakati tofauti na wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya maskini na wananchi kwa ujumla katika Halmashauri za Wilaya ya Geita, Chato na Bukombe Mkoa wa Geita.
“Nimetembelea na kukagua miradi iliyopangwa, kwa ujumla nimefurahi sana kwa utekelezaji mzuri mathalani shule na vituo vya afya vimejengwa kwa viwango vizuri.
“ Hivyo, nitoe rai kwa halmashauri zote nchini na wananchi kuhakikisha miradi hiyo inatunzwa kwa kuwa ni sehemu ya chaguo na vipaumbele vya wananchi wenyewe katika maeneo yao,” amesema.
Amewasisitiza waratibu wa TASAF katika Mkoa wa Geita kuhakikisha shule na vituo vya afya vinavyojengwa kupitia mradi huo vinawekewa miundombinu ya maji na umeme na kuweka madawat,i ili madarasa hayo yaanze kutumika.