Watakiwa kutunza miundombinu ya maji

WANANCHI zaidi ya 2,000 wa Kijiji cha Mushabaiguru wilayani Karagwe, mkoani Kagera wameondokana na changamoto ya upatikanaji  wa maji safi na salama, baada ya serikali kutekeleza mradi wa maji kijijini hapo uliogharimu zaidi ya Sh milioni  190.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila, amefungua mradi huo na kuwasisitiza wananchi kulinda miundombinu ya maji, ikiwemo kuchangia gharama za maji, pale bili inapoletwa nyumbani kwao na kwenye vituo vya kuchota maji, ili kufanya mradi huo kuwa endelevu na kuendelea kuwa kumbukumbu kwao na vizazi vijavyo.

Alitoa wito kwa kamati za watumia maji zinazoundwa kijijin hapo, uongozi wa serikali ya kijiji, kuhakikisha wananchi hawavamii vyanzo vya maji,hawaingizi mifugo pamoja na kulima karibu na vyanzo vya maji.

“Serikali inatumia fedha nyingi kusogeza huduma ya maji kwa wananchi, ,Wilaya ya Karagwe  ni miongoni mwa wilaya ambazo wananchi wake wamepata madhara na maumivu makubwa sana katika utafutaji wa maji,” amesema Chalamila.

Meneja wa wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Wilayani humo, Yusto  Mtabuzi  amesema mradi huo umekamilika na tayari  familia zimeunganisha maji katika nyumba zao na wengine wakitumia vituo vya kuchota maji.

Alisema kuwa serikali inaendelea kutekeleza miradi ya maji na safi na salama na kwa Sasa wakazi wa Karagwe wanaoishi vijijini wanapata maji safi na salama kwa asilimia 74.

Habari Zifananazo

Back to top button