Watakiwa kutunza vyanzo vya maji

WANANCHI wa Kata za Katoma na Karabagaine, Halmashauri  ya Bukoba  mkoani Kagera, wamehimizwa kuhakikisha wanalinda na kutunza chanzo cha maji Kyeiringisa kwa kutofanya shughuli za kibinadamu katika chanzo hicho.

Meneja wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (Ruwasa)  Bukoba Vijijini, Mhandisi Evaristo Mgaya aMEtoa wito huo baada ya mwenge wa uhuru kuzindua mradi wa maji Kashenge –Ilogero uliogharimu zaidi ya Sh milioni 768.

Mradi huo utakuwa na uwezo wa kuhudumia wananchi zaidi ya 7,000 katika vijiji vya Kashenge na Irogelo na kufanya mtandao wa maji katika Kata Katoma kupatikana kila kijiji.

Amesema kuwa chanzo hicho ni kikubwa na kinategemewa na wananchi wa kata hizo  mbili pamoja na kata nyinginezo, hivyo suala kubwa ni kukitunza kama mboni ya jicho lao la kujiepusha na kukata miti, kuchoma moto, kulima na kujenga.

“Serikali inatumia gharama kubwa sana kuwasogezea wananchi huduma za maji, lakini wengi wao wananchoangalia ni ile fedha iliyotumika, kinachopaswa kulindwa hapa na kuogopwa zaidi ni chanzo cha maji, “amesema Mgaya.

Amesema mradi huo ni mkombozi wa tatizo la upatikanaji wa maji, ambalo limewakumba wananchi wa vijiji hivyo kwa muda mrefu, hivyo ni matarajio ya serikali kuwa mradi huo utakuwa kichocheo cha maendeleo kwa wananchi.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi wa kata ya Katoma walisema kuwa kuzinduliwa kwa mradi huo kutawasaidia kuepukana na adha waliyokuwa wanapata, kwani iliwalazimu kuamka usiku sana kwenda kuchota maji kwenye vyanzo vya asili.

Kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa Abdallah Shaib Kaim, aliwasisitiza wananchi kulinda na kuitunza miradi ambayo inajengwa, ili kutimiza azma ya serikali ya kuhakikisha inatatua changamoto ya maji na kumtua mama ndoo kichwani, kwani serikali haipendi kuona wananchi wake wanateseka .

Habari Zifananazo

6 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button