Watakiwa kuzidisha mapambano kupinga ukatili

WADAU wa kupinga ukatili mkoani Kigoma, wametakiwa kutimiza wajibu wao kikamilifu katika kutekeleza mpango huo kwani hali bado ni mbaya kwa matukio ya ukatili nchini.

Katibu Tawala wa Mkoa Kigoma Albert Msovella, alisema hayo akifunga mkutano wa siku moja wa wadau wa kupinga ukatili mkoani humo kutathimini utekelezaji wa mpango wa Taifa wa kutokomeza ukatili (MTAKUWA) na hatua za kuchukua kukabili hali hiyo.

Katika hotuba iliyotolewa kwa niaba yake na Katibu Tawala wa Wilaya Buhigwe mkoani Kigoma, Peter Masindi alisema kuwa pamoja na kuwepo kwa mafanikio katika utekelezaji wa MTAKUWA lakini hali ya ukatili nchini na mkoa Kigoma bado mbaya.

Katibu Tawala huyo wa Mkoa Kigoma alisema kuwa kila mmoja kwa nafasi yake anapaswa kubeba ajenda ya jambo hilo kama jambo lake binafsi katika kuwalinda watoto na wanawake, huku akitoa rai kwa wazazi kuhakikisha ulinzi na matunzo ya watoto wao.

Akichangaia katika majadiliano ya kikao hicho Padri Castuc Rwegoshora kutoka Kanisa Katoliki Jimbo la Kigoma, alisema kuwa bado wazazi hawajaipa dini nafasi kubwa katika kutoa mafundisho na kusimamia malezi ya watoto wao kidini, ndiyo maana bado vitendo viovu vya ukatili vinaendelea kwenye jamii.

Naye Mkurugenzi wa Taasisi isiyo ya kiserikali ya Women Promotion Centre (WPC), Martha Jerome alisema kuwa dini ikipewa nafasi kubwa ya kusimamia malezi ya watoto na kutoa nasaha kwa jamii kila wakati inaweza kusaidia kupunguza hali ilivyo sasa na watu kuishi kwa hofu ya Mungu.

Mkuu wa dawati la jinsi la jeshi la polisi mkoa Kigoma, Michael Mjema alisema kuwa tangu kuanzishwa kwa madawati hayo na kuanza kutekelezwa kwa MTAKUWA kumekuwa na mafanikio makubwa kwa jamii kutoa taarifa kwa matukio ya ukatili yanayotokea na kuwezesha mamlaka mbalimbali kuchukua hatua.

Hata hivyo Mjema alisema kuwa bado wazazi na familia zimekuwa kikwazo kwa mashauri mengi kushindwa kufika mwisho na watuhumiwa kushindwa kuchukulia hatua kutokana na familia kukaa kulimaliza shauri hilo nyumbani na wakati mwingine kuharibu ushahidi au kushindwa kutokea kabisa mahakamani kesi inapofikishwa huko.

Habari Zifananazo

Back to top button