Watakiwa kuzingatia sheria utunzaji mazingira

KATIBU Tawala wa Wilaya ya Tanganyika, mkoani Katavi, Geofrey Mwashitete amewataka wananchi wa wilaya hiyo kuzingatia sheria za utunzaji wa mazingira, ikiwemo hifadhi za Taifa, misitu, vyanzo vya maji na milima kwa kutokata miti wala kuanzisha makazi na shughuli za uchumi.

Mwashitete ametoa maagizo hayo katika uzinduzi wa upandaji miti katika mfumo wa ikolojia ya Mto Katuma, uliofanyika Kijiji cha Kapanga wilayani humo kwa kuandaliwa na asasi ya Green Agenda-Tanzania.

Amewataka wananchi na serikali kuungana, ili kuhakikisha kwamba Mto Katuma pamoja na mito mingine inakuwa salama, huku akisema kila kaya ihakikishe inapanda miti 10 kwa kuwa ni agizo la serikali kuu.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Ofisa Maliasili na uhifadhi wa mazingira, Bruno Nicholaus amesema wamependekeza kupanda mti aina ya mkangazi (Khaya anthotheca), kwa sababu mti huo ni miongoni mwa miti iliyo katika hatari ya kupotea duniani.

“Tumechagua mti huu kwasababu tumeona vyanzo vyetu vya maji na kingo za maji zinaharibika, mti huu ni mzuri kwa ajili ya uzalishaji wa mbao ngumu pamoja na kutunza vyanzo vya maji, na lengo kubwa kwa sababu mti huu hautumii maji mengi isipokuwa unatunza maji,” amesema.

Awali akitoa taarifa kwa mgeni rasmi, Mkurugenzi wa asasi ya Green Agenda-Tanzania, Josiah Severre, alisema lengo la mradi huo ni kurudisha upya uoto wa asili katika mfumo wa ikolojia ya Mto Katuma, ambayo iliharibiwa vibaya kutokana na shughuli za kibinadamu, ikiwemo kilimo kisichozingatia utaratibu, kulima kwenye kingo za mto, ukataji miti, upanuzi wa ujenzi wa makazi na ufugaji holela.

Alisema mradi huo wa upandaji miti wanashirikiana na halmashauri hiyo kupitia shule ya Msingi Katuma na unafadhiliwa na taasisi ya TNC, kupitia programu ya Tuungane  na unalenga kuotesha miti ipatayo 200,000 katika mwaka 2022/23 katika Vijiji vya Kapanga, Katuma, Kamilala, Mnyagala, na utakuwa endelevu katika vijiji vingine vinavyozunguka mto Katuma.

Habari Zifananazo

Back to top button