Watakiwa kuzingatia usafi wa mabucha

WADAU walio kwenye mnyororo wa thamani wa mazao yatokanayo na mifugo katika Mkoa wa Katavi , wametakiwa kufuata sheria, kanuni na taratibu ikiwemo wauzaji wa nyama kwa kuboresha usafi katika mabucha yao, na kuepuka matumizi ya magogo na vyuma vyenye kutu ili kulinda afya ya walaji.

Hayo yamesema na Afisa Mfawidhi wa Bodi ya Nyama Kanda ya Magharibi, Joseph Kulwa wakati wakifanya ukaguzi, usajili na utambuzi wa mabucha katika mkoa huo ambapo amesema vitu walivyovibaini ni pamoja na wafanyabiashara wa nyama kuongeza mabucha bubu ambayo hayajasajiliwa ikiwa ni pamoja na kupima afya zao.

Kulwa amesema pamoja na kubaini vitu hivyo bado wanaendelea kuwapa elimu pamoja na kuzingatia sheria ya tasnia ya nyama sheria namba 10 ya mwaka 2006 ambayo inawataka watambulike kwa kusajiliwa, huku wakibaini mabucha sita ambayo hayajasajiliwa.

“Wadau wetu bado wanaendelea kutotii maelekezo ya sheria ilivyo kwa kwenda kinyume na sheria inavyo taka, bado mabucha nimachafu, upimaji wa afya tatizo, bado matumizi ya magogo yapo matumizi ya nondo chafu yapo na uuzaji wa nyama ambazo hazijakaguliwa machinjioni” amesema na kuongeza “Sisi tunatoa elimu, pale inapoladhimu tunawapiga faini ili pengine kuwakumbusha kwamba nitakwa la kisheria wanatakiwa wafuate utaratibu kadri ya sheria inavyotaka,” amesema Kulwa.

Nae msimamizi wa machinjio ya Mpanda hoteli Juma Gilibert, amesema machinjio hiyo ilikua ikikabiliwa na changamoto ya uzio na kusababisha muingiliano wa watu wasio husika na wanyama wengine kama vile mbwa hivyo serikali imeendelea kutenga bajeti kwa ajili ya kukamilisha utatuzi wa changamoto hizo.

Nae Frank Mwita ambae ni mfanyabiashara wa nyama amesema usafi na uboreshaji wa mabucha huchangia kuongeza kipato na kujali afya za walaji huku akishauri wengine kuacha kutumia magogo na nondo zenye kutu.

Habari Zifananazo

Back to top button