WAKAZI wa Wilaya ya Muleba wametakiwa wasijichukulie sheria mkononi na kujiepusha na vitendo vya mauaji, badala yake watumie vyombo vya sheria, ili kupata haki inayostahili.
Hakimu mkazi mfawidhi wa wilaya ya Muleba, Daniel Nyamkerya, alisema wilaya hiyo imekuwa ikikumbwa na visa vya mauaji, ambapo wananchi wanauana wenyewe kwa wenyewe bila kufika katika vyombo vya sheria, jambo ambalo linachochea chuki kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
“Moja ya changamoto kubwa iliyopo katika Wilaya ya Muleba ni wananchi kujichukulia sheria mkononi bila hata kuhoji wala kufika katika vyombo vya sheria wengine hawataki kufika hata vyombo vya maamuzi vilivyopo jamii.
“Unakuta mtu anamtuhumu mwenzake kabla ya kuthibitisha tuhuma zake anajipanga kumuua, hili jambo linachochea chuki kila siku wananchi lazima tujielimishe na tutumie vyombo vilivyoundwa kisheria,” alisema Nyamkerya.
Alisema changamoto nyingine ni kuwa wilaya hiyo inakata 45 katika kata hizo kuna visiwa 39, lakini mahakama ambazo zinazofanya kazi ni tisa, ambapo wafanyakazi wa mahakama hizo hulazimika kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
“Baadhi ya wananchi hutembea umbali mrefu kufuata huduma za mahakamani, hivyo wengine hukata tamaa ya kupeleka malalamiko uwaze kujichukulia hatua, lakini watendaji wetu pamoja na kuwa mahakama ni chache wanajitahidi kufika kuwasikiliza.
“Wapo baadhi ya wananchi ambao anajua kabisa anapaswa kuja kusikiliza kesi yake na anajua hakimu siku hiyo yupo, lakini bado hafiki mahakamani, ndugu wananchi tunaomba mfike mahakamani, ili mpate hata elimu ya sheria bila gharama yeyote,”alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Muleba Dk Abel Nyamahanga, amekemea vitendo vya mauaji, ambapo alisema kuwa licha ya kuwa ameteuliwa hivi karibuni, lakini tayari amepokea taarifa kuwa wilaya hiyo, inaongoza kwa vitendo vya mauaji mkoani Kagera.
Alisema pia wananchi wanapaswa kupunguza muda wa kwenda mahakamani kwa kesi ambazo sio za jinai, huku akidai kuwa vyombo vilivyoundwa katika jamii vina mchamgo mkubwa wa kuleta usuluhishi kati ya mlalamikaji na mlalamikiwa, lakini wakiona hawajaridhika basi wafike mahakamani.