Watangazaji waongoza kuharibu Kiswahili
DAR ES SALAAM: Watangazaji wa radio na runinga wametajwa kuongoza kukidhalilisha Kiswahili huku wamiliki wa vyombo vya Habari wakilaumiwa kuajiri watu wasio na taaluma ya uandishi wa habari ambao wanachangia kuidhalilisha taaluma hiyo.
Hayo yamesemwa na Wakongwe wa Habari ambao ni waanzilishi wa Radio Tanzania (RTD) sasa TBC walipokwenda kutambulisha chama chao kwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye.
Wakongwe hao wakiongozwa na Suleiman Kumchaya, Tido Mhando, Debora Mwenda ‘Mama na Mwana’ Edda Sanga, Rose Haji, Penzi Nyamungumi, Zuhura Mdungi, Abdukadir Ndeo, Angalieni Mpendu na Godliver Rweyemamu pia wamemueleza Waziri Nape dhamira yao ya kuanzisha chuo cha mafunzo kwa waandishi wa habari pamoja na kituo cha utangazaji wakiwa na kauli mbiu ya ‘tusizikwe tungali hai’
Angalieni Mpendu amesema vyombo vya habari vimekuwa vikitumia lugha za mitaani akitolea mfano neno dada linavyotumiwa vibaya kwa kuitwa Mdada.
“Hakuna neno mdada kwenye Kiswahili kuna dada, lakini wao utasikia Mmama badala ya mama, Maokoto badala ya Pesa, nipe tano badala ya umenifurahisha.
“Studio zimegeuka vijiwe vya mipasho na kuzungumzia watu inasononesha sana, Kiswahili kinaonekana hakina mwenyewe, lugha inakuwa sawa lakini sio kwa aina hii.”amesema Mpendu.
Kwa upande wa Edda Sanga amesema pamoja na kwamba kitabu cha zama zao kimefungwa na sasa kuna kitabu cha zama mpya, lakini umakini unahitajika hivyo ni wajibu wao kama wakongwe wa tasnia ya habari kuwarudisha waandishi wa habari hususani watangazaji kwenye mstaari ulionyooka, hawatakubali kuona tasnia waliyoipambania kwa wivu mkubwa ikibanangwa.
“Media zimekuwa na maudhui mengi ya kupotosha jamii badala ya kuelimisha, wanakidhalilisha Kiswahili ndio maana tunakuja na mpango huu tuwafundishe namna ya kuandaa Makala za vipindi mbali mbali vya kuelimisha jamii na hata namna ya kuandika ‘script’; ……. “wengi tu kwa sababu ni maarufu wanachukuliwa mtaani haya kaa hapa tangazaa hawana hata a, b,c za uandishi wa habari ndio maana tunaona maudhui mengi yasiyofaa.
”amesema.
Nae, Waziri Nape alipongeza mpango huo na kuwahidi kuwapa ushirikiano na kwamba kila wanachokifanya serikali inabaraka zake na watasaidia chama hicho kukua na kuleta mapinduzi katika tasnia ya habari ili iheshimike kama zamani.