SERIKALI imesema hadi kufikia Julai 31, 2023 jumla ya Watanzania 11,242,736 wamepewa vitambulisho sawa na asilimia 55 ya lengo la kuwapatia wananchi 20,294,910 wanaostahili kupewa.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamis, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Esther Matiko aliyetaka kujua ni asilimia ngapi ya Watanzania wameandikishwa na kupatiwa Kitambulisho cha Taifa.
Akijibu swali hilo kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Naibu Waziri Khamis amesema mpango wa Serikali ni kuwagawia vitambulisho Watanzania 9,052,174 waliobaki ifikapo mwezi Machi, 2024.