WATANZANIA 50 ambao walijiorodhesha kama sehemu ya waomba hifadhi, ili kupewa hadhi ya ukimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), wamenyimwa hadhi ya ukimbizi na kurudishwa nyumbani.
Mratibu wa Idara ya Wakimbizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Kanda ya Magharibi, Nashon Makundi alisema hayo akitoa taarifa kwa waandishi wa habari akieleza maendeleo ya wakimbizi wa DRC, ambao wameendelea kuingia nchini.
Makundi alisema kuwa Watanzania hao wana uhusiano wa kifamilia na wakimbizi hao wa DRC, hivyo taratibu za nchi haziwezi kuwaruhusu kuishi kambini kama wakimbizi, wakati wanayo miji yao waliyokuwa wakiishi kabla ya kuingia kwenye uhusiano.

Alibainisha kuwa baadhi ya Watanzania hao hawana nyaraka (vyeti vya ndoa) kuwathibitishia uwepo wa ndoa baina yao na wenzao hao wa DRC, hivyo bado taratibu za kuwapa hadhi ya ukimbizi na kuishi kambini kwa maana ya kuwafuata wake au waume zao hazikubali.
Akieleza mtiririko wa wakimbizi kuingia nchini, alisema kuwa hadi sasa waomba hifadhi 6,021 wamepokelewa na kuandikishwa, ambapo kati yao zaidi ya 3000 tayari wameshapelekwa kwenye kambi ya wakimbizi wa DRC ya Nyarugusu, iliyopo Kasulu mkoani Kigoma.
” Kwa sasa idadi ya waomba hifadhi wanaoingia nchini imepungua sana na wanaoingia taratibu za kuwahoji zinaendelea kama kawaida,” alisema Mratibu huyo wa wakimbizi.
Baadhi ya wakimbizi wa DRC waliozungumza na waandishi wa habari wameeleza hali tete ya usalama ilivyokuwa na kulazimika kukimbia na kuomba hifadhi nchini Tanzania.
Mmoja wa waomba hifadhi hao, Alaki Tulale kutoka Butembo Jimbo la Kivu ya Kusini, alisema kuwa amekimbia baada ya kuvamiwa na waasi wa M23 kwenye makazi yao, ambao wamekuwa wakiteka vijana na kuwataka kujiunga na kambi zao sambamba kuua watu.
Alisema kuwa nyumbani kwao Mkoa Fizi, ambako wazazi wake na ndugu zake walikuwa wakiishi hali ni mbaya na hajui hadi sasa ndugu zake wana hali gani, lakini anashukuru yeye binafsi yuko salama hapa nchini.