Watanzania changamkieni fursa za uwekezaji

MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango amewataka wawekezaji wa ndani kutumia vizuri na kikamilifu mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyowekwa na serikali kuanzisha miradi mbalimbali ambayo itawezesha kutoa ajira kwa Watanzania.

Dk Mpango alisema hayo wilayani Kasulu mkoani Kigoma wakati akifungua Hotel ya Bwami Dubai iliyojengwa na mwekezaji binafsi na kusema kuwa serikali inasisitiza Watanzania kutumia fursa hiyo kuwekeza kwa kadri wanavyoweza.

Alisema kuwa serikali ya awamu ya sita imeondoa kodi na tozo ambazo zilikuwa kero kwa wafanyabiashara na wawekezaji kwenye sekta mbalimbali ili kuweza kutumia mitaji waliyonayo kuanzisha shughuli mbalimbali ambazo zitakuwa kichocheo katika kukuza uchumi wa nchi.

Makamu wa Rais alisema kwa sasa sekta binafsi ndiyo inayotoa ajira kwa wingi kwa watu kujiajiri au kuajiri watu wengine na hiyo yote inatokana na mazingira mazuri ambayo serikali imeyaweka kuwezesha watu wengi kuanzisha shughuli za uwekezaji kwenye kilimo, madini, viwanda na shughuli nyingine ambazo zitazalisha ajira.

Akizungumzia uwekezaji kwa Mkoa Kigoma alisema kuwa serikali imedhamiria kuweka mazingira mazuri kwa mkoa huo kuwezesha kuvutia uwekezaji kwa kuimarisha miundo mbinu ya barabara, reli na usafiri wa anga, upatikanaji wa umeme wa uhakika, huduma za afya na huduma nyingine za msingi zinazohitajika ambazo zinavutia wawekezaji hivyo amewataka wananchi wazawa wa Kigoma kurudi kuwekeza mkoani humo.

Mkurugenzi wa hoteli hiyo, Evance Chocha alisema kuwa mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyowekwa na Raisi Samia Suluhu Hassan ndiyo yaliyomfanya kujenga hoteli hiyo iliyogharimu kiasi cha Sh bilioni 1.6 ambayo ina vyumba 36 na ukumbi wenye uwezo wa kuchukua watu 50.

Chocha alisema kuwa katika uwekezaji wake hadi sasa ameshatoa ajira kwa Watanzania 45 huku hoteli hiyo ikiwa na fursa kubwa ya kukuza uchumi wa Kigoma kwa kodi na maununuzi mbalimbali ambayo yatakuwa yanafanyika kwa ajili ya matumizi ya hoteli hiyo.

Habari Zifananazo

Back to top button