Watanzania kupewa elimu ya fedha kuchangia maendeleo

WIZARA ya Fedha na Mipango itakuwa na Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa kwa wiki moja kwa lengo la kutoa elimu ya kifedha kwa Watanzania nchini.

Akizungumza jijini Dodoma juzi Kamishna wa Uendelezaji wa Sekta ya Fedha katika Wizara ya Fedha na Mipango, Dk Charles Mwamwaja alisema maadhimisho hayo yatatumika katika kufaidika na fursa ya elimu ya fedha ni jambo msingi.

Maadhimisho hayo yanabainisha namna wizara inavyofanya usimamizi wa sekta ya fedha katika kujenga mazingira mazuri ya kisera, kisheria, kikanuni na kitaratibu ili kuchangia maendeleo ya fedha.

“Maadhimisho hayo ya wiki moja ya huduma za kifedha kitaifa yatafanyika katika Jiji la Mwanza kuanzia Novemba 21-26, 2022,” alisema.

Maadhimisho hayo hufanyika kila mwaka na yalianza mwaka jana Dar es Salaam katika Viwanja vya Mnazi Mmoja kati ya Novemba 8-14.

Maonesho ya mwaka huu yana kauli mbiu, ‘Elimu ya fedha kwa maendeleo ya watu’.

Maadhimisho ya mwaka huu ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkuu wa sekta ya fedha wa kuongeza idadi ya nguvukazi ya watumiaji huduma rasmi za kifedha kutoka asilimia 48.6 ya sasa.

Mambo ya msingi yatakayofanyika katika maadhimisho ni pamoja na kujenga uelewa na weledi kwa umma katika matumizi sahihi ya huduma za fedha zinazotolewa ili kujenga uchumi na kuondoa umasikini.

Alisema lengo ni wananchi wapate elimu kuboresha maisha kupitia fursa zinazotolewa na wizara kwani mpango ni kuhakikisha kwamba ifikapo mwaka 2025 zaidi ya asilimia 80 wawe wamepata kwa sasa ni asilimia 60.

Aliwataka wananchi wa Mwanza na mikoa jirani Shinyanga, Simiyu, Kagera, Mara, Geita kufika na kushiriki katika maonesho hayo kuleta mabadiliko chanya katika kuleta maendeleo yao.

Katika maadhimisho hayo mambo yatakayofanyika ni kuainisha utoaji elimu kwa umma kuimarisha utamaduni wa kuweka akiba, kukopa na kulipa madeni na kuongeza mchango katika sekta ya fedha kwenye ukuaji uchumi.

Nyenzo ya kufundishia elimu ya fedha imeandaliwa kupitia kitabu ambacho kimeandaliwa kwa lugha nyepesi.

Masuala mengine ni pamoja na kusimamia fedha binafsi, kuweka akiba, kupanga na kuchukua, namna ya kuchukua mikopo, uwekezaji, huduma za bima na hati fungani.

Takwimu zilizopo zinaonesha kwamba asilimia 48.6 ya Watanzania hawajafikiwa na huduma za kifedha. Wengi kupata elimu uelewa ili kufanya usimamizi mzuri na matumizi ya elimu.

“Huduma ya fedha kitaifa kujenga uchumi na kupambana na uadui masikini, kuimarisha ufanisi huduma za kifedha na masoko ya dhamana. Kuongeza upatikanaji wa huduma za fedha,” alisema.

Alisema kutakuwa na mabanda takribani 150 yenye wataalamu waliojipanga kutoa elimu, semina, mijadala na kutoa elimu kupitia mitandao ya kijamii ili elimu hiyo kuwafikia Watanzania wengi zaidi.

Habari Zifananazo

Back to top button