TANZANIA leo inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya vyama vya ushirika duniani ikiwa na vyama 7,300 vya ushirika nchini vyenye jumla ya wanachama milioni 8.3.
Maadhimisho hayo kitaifa yatafanyika mkoani Tabora kwa kaulimbiu isemayo ‘Ushirika kwa Maendeleo Endelevu.’ Hayo yamebainishwa na Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dk Benson Ndiege alipozungumza na HabariLEO jana.
Dk Ndiege alisema walianza maadhimisho hayo tangu Juni 26, mwaka huu na kuhitimishwa leo na kuwa hii ni mara ya 27 maadhimisho hayo kufanyika nchini lakini ni mara ya tatu mfululizo kufanyika mkoani Tabora.
Alisema wameamua kufanya maadhimisho hayo mkoani Tabora mara tatu mfululizo baada ya kugundua kuwa mkoa huo ulikuwa nyuma kwa mwamko kuhusu masuala ya ushirika, hivyo lengo lao ni kuhamasisha wananchi kuona umuhimu wa kujiunga na vyama vya ushirika.
Kwa mujibu wa Dk Ndiege hivi sasa Tanzania ina vyama 7,300 vya ushirika vyenye jumla ya wanachama milioni 8.3. Alisema vyama vya ushirika vimegawanyika katika makundi mbalimbali na vina uwezo tofauti na kubainisha kuwa kwa upande wa Saccos kuna vyama vina uwezo wa mtaji hadi Sh bilioni 60.
“Tunaishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuuongezea nguvu ushirika ikiwemo kutuongezea watumishi, vifaa na bajeti. Tumejitahidi kudhibiti vitendo vya ubadhirifu vilivyokuwa vinapigiwa kelele na tunatarajia vitakwisha kabisa,” alisema.
Dk Ndiege alisema matarajio yao ni kuifanya sekta ya ushirika kuwa kinara katika kuchangia ukuaji wa uchumi pamoja na kuongeza ajira, kuongeza uhakika wa masoko na upatikanaji wa pembejeo na mitaji. Alisema mgeni rasmi katika kuhitimisha maadhimisho hayo leo anatarajiwa kuwa Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe.
Muungano wa Kimataifa wa Ushirika (IAC) ulikuwa ukiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Ushirika kila Jumamosi ya kwanza ya mwezi Julai tangu mwaka 1923. Ilipofika mwaka 1992, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilitangaza azimio la kuifanya Jumamosi ya kwanza ya Julai kuanzia mwaka 1995 kuwa siku rasmi ya Kimataifa ya Ushirika.