Watanzania milioni 32.7 wachanja Covid-19

TAKRIBANI Watanzania milioni 32.7 sawa na asilimia 53.4 wamekamilisha kuchoma chanjo dhidi ya ugonjwa wa Covid-19.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema bungeni Dodoma jana wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za bajeti hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/24.

Alisema hadi kufikia Machi mwaka huu dozi milioni 46.8 za chanjo ya ugonjwa wa corona zimepokelewa na kusambazwa na dozi milioni 39.1 sawa na asilimia 84 zimetumika.

Alieleza kuwa Wizara yake imeratibu upatikanaji wa chanjo dhidi ya ugonjwa wa virusi vya corona kupitia mpango wa kidunia kuhakikisha nchi zinapata chanjo ya ugonjwa huo na misaada kutoka nchi rafiki.

“Hadi kufikia Machi, 2023 jumla ya dozi milioni 46.8 zilikuwa zimepokelewa na kusambazwa ambapo dozi milioni 39.1 sawa na asilimia 84 zimetumika hadi sasa,” alisema na kuongeza kuwa wizara inaendelea kuratibu utoaji wa chanjo dhidi ya ugonjwa huo wa Covid-19 kupitia vituo vya kutolea huduma za afya vya umma na binafsi, huduma za mkoba na kampeni.

Alisema vituo vya kutolea huduma 7,200 vinatoa huduma ya chanjo ya ugonjwa huo hapa nchini na kuwa hadi kufikia Machi 2023 Watanzania milioni 32.7 ambao ni sawa na asilimia 53.4 ya Watanzania wote walikuwa wamekamilisha chanjo dhidi ya ugonjwa huo.

Ummy alisema katika kipindi cha Julai 2022 hadi Machi 2023, kumekuwa na wastani wa visa 302 kwa mwezi bila kifo ikilinganishwa na kipindi kama hiki kwa mwaka 2021/22 ambapo kulikuwa na wastani wa visa 1,557 na vifo 43 kwa mwezi.

Kuhusu ugonjwa wa saratani, waziri huyo alisema serikali imeendelea kuwalinda wasichana wenye umri wa miaka 14 dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi kwa kununua na kusambaza chanjo ya ugonjwa huo iitwayo Human Papilloma Virusi (HPV) dozi 763,500.

Alisema katika kipindi cha Julai 2022 hadi Machi 2023, wasichana 535,708 wenye umri wa miaka 14 ambao ni walengwa wa huduma za chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi walipatiwa chanjo.

Habari Zifananazo

Back to top button