Watanzania wahamasishwa kutunza amani
KAMATI ya Amani ya viongozi wa dini Mkoa wa Mwanza, wameiomba serikali kuendelea kuandaa makongamano kwa kuungana na viongozi wa dini kwa lengo la kutoa elimu ya ufafanuzi kuhusu mkataba wa bandari.
Ombi hilo limetolewa leo na Mwenyekiti mwenza wa Kamati ya Amani ya viongozi wa dini Mkoa wa Mwanza, Charles Sekelwa wakati wa mkutano na wandishi wa habari .
“Sisi viongozi wa kamati ya amani ya viongozi wa dini Mkoa wa Mwanza tunaiomba serikali ituletee kongamano hili katika mikoa yetu ya Kanda ya Ziwa kwa haraka, ili viongozi wetu waweze kupata uelewa wa kutosha kuhusiana na mkataba wa bandari,” amesema Sekelwa.
Amewaomba Watanzania wote kupitia dini zao,taasisi na vyama vya siasa kuendelea kuilinda na kuitunza amani ya nchi kwa kuwa amani ikitoweka hakuna atakayebaki salama.
Sekelwa amesema suala la uwekezaji na uendeshaji wa huduma za bandari, linahitaji wadau wakubwa kama Jumuiya ya biashara na shirikisho la wenye viwanda nchini.
“Mkataba huu wa bandari tayari bunge letu limeshajadili na kupitisha kwa niaba ya wananchi, kwani kwa sasa hao ndio wabunge wetu na hilo ndio bunge letu,” amesema Sekelwa.
Naye Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke amesema kamati ya dini ya mkoa wa Mwanza inalo jukumu kubwa la kudumisha amani.
Amesema katika mitandao ya kijamii kumekuwa na watu wengi wenye msimamo tofauti sana kuhusiana na uwekezaji wa bandari.
Amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa usikivu na uvumilivu wake kuhusu suala la bandari, kwa kuwa mpaka sasa hajatoa tamko lolote na anaendelea na majukumu yake ya kuwatumikia Watanzania.