DAR ES SALAAM: KAIMU Meneja Mahusiano wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Grace Michael amesema muitikio wa Watanzania kutaka huduma za NHIF umekuwa mkubwa, ni kiashirio kuwa elimu juu ya bima ya afya imewafikia.
Meneja huyo ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba 2024) yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere vilivyopo Barabara ya Kilwa.
“Leo ni siku ya 10 tangu kufunguliwa kwa maonesho haya Juni 28, lakini kufikia siku ya 5 hadi leo tumekuwa tukihudumia wateja wasiopungua 400 kwa siku,” amesema Grace.
SOMA: Hakuna atakayekosa huduma NHIF
Amesema kutokana na muitiko wa Watanzania ni dhahiri maamuzi ya kuwa na bima ya afya kwa kila mmoja limekuja katika wakati muafaka.
Amesema, pamoja na muitikio huo bado dhamira yao ya kutoka maofisini na kuwafata Watanzania kuwaelimisha inaendelea.
“Wote tunaona juhudi na kiu ya Mhe. Rais Samia kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora ya afya, sasa sisi ni kina nani tusimuunge mkono Rais,” amehoji kiongozi huyo.
Mwezi Desemba 2023, Muswada wa Bima ya Afya kwa wote ulisainiwa na Rais Samia Suluhu Hassana baada ya kupitishwa bungeni kwa asilimia 100 ya kura za wabunge.
Utekelezaji wa muswada huo unatarajiwa kuanza mwaka huu wa fedha, ambapo inatarajiwa hakuna Mtanzania yeyote atakayekosa huduma kwa sababu ya fedha kwani kadi yake itamuwezesha kupata huduma ya afya.
SOMA: Mpango wa Afya kwa Wote (UHC)
Taarifa kutoka Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) inabainisha kuwa idadi ya watu ulimwenguni bado hawawezi kupata huduma muhimu za afya.
“Takriban watu milioni 100 bado wanaendelea kusukumwa katika umaskini mkubwa (yaani wanaishi kwa Dola 1.90 au chini yake kwa siku) kwa sababu wanalazimika kulipia huduma za afya,
“Watu zaidi ya milioni 800 (karibu asilimia 12 ya idadi ya watu ulimwenguni) walitumia angalau asilimia 10 ya bajeti zao za nyumbani kulipia matibabu,” imeeleza taarifa hiyo na kubainisha kuwa
Nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa wamekubali kujaribu kufaulisha mpango wa afya kwa wote (UHC) kufikia mwaka 2030, kama sehemu ya Malengo ya Ustawi Endelevu.