“Watanzania wana shauku kutumia SGR”

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imesema Watanzania wanayoshauku kubwa ya kuona matumizi ya treni ya Mwendokasi (SGR), inaanza kufanya kazi.

Kutokana na shauku hiyo, kamati imeitaka serikali kuongeza kasi ya kukamilisha maeneo machache yaliyobakia ili uwekezaji uliofanyika uanze kuonesha manufaa .

Mwenyekiti wa Kamati hiyo,Dk  David Mathayo alisema hayo mjini Morogoro wakati wa ziara ya kawaida ya kikazi kwa ajili ya kukagua  utekelezaji mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa KV 220 kwa ajili ya uendeshaji wa Treni ya Mwendokasi (SGR).

Kamati hiyo imesema utekelezaji wa mradi wa awamu ya pili kwa kipande cha Msamvu hadi Ihumwa uliofikia asilimia 99, serikali inapaswa iendelee kusukuma kasi kwa  Shirika la Umeme (TANESCO) ikamilishe asilimia moja iliyopakia.

“Kwa sasa tunaishauri serikali iongeze kasi (speed) kidogo ili tumalizie huu mradi  na tuendelee na mambo mengine …tuone kweli kwa sasa inafanya kazi , Reli inapitisha vichwa na mabehewa ya abiria na mizigo …tunataka tuone uwekezaji tulioufanya una manufaa.”amesema Dk Mathayo

Kamati hiyo imeitaka serikali kuendelea kutoa elimu na tahadhari kwa wananchi kuhusu hatari ya kupitia meneo yaliyozungushiwa uzio na kupitisha mifugo karibu na njia ya reli ya mwendokasi ili kuepusha majanga.

Dk Mathayo amesema ni vyema kwa serikali kuu ikishirikiana  na serikali za mitaa kuzidi  kutoa elimu ya  tahadhari kwa ajili ya kuzuia ajali ambazo zinaweza kutokea .

“ Serikali tuwatumie watendaji wa vijiji, kata , wenyeviti wa vijiji, mitaa na vitongoji wasaidiane na serikali kuu kuendelea kutoa elimu na tahadhari kwa wananchi wanaopita maeneo ambayo yamewekewa uzio ikiwa na wafugaji kuacha tabia ya kupitisha mifugo kwa  ajili ya kuzuia ajali ambazo zinaweza kutokea “ amesema Dk Mathayo.

Habari Zifananazo

Back to top button