Watanzania wanaosoma China waonywa ulevi, ‘unga’

UBALOZI wa Tanzania nchini China, umewataarifu wanafunzi wote wa Tanzania wanaosoma nchini humo kuwa mipaka iko wazi na wanaweza kurejea vyuoni mwao, lakini ni vyema wakapata maelezo juu ya kanuni na masharti ya ukaazi wanayotakiwa kuyazingatia katika miji na vyuo vyao.

Pia ubalozi umewashauri wanafunzi hao kuishi kwenye hosteli za vyuo badala ya kupanga mitaani, huku wakionywa kuachana na aina zote za unywaji pombe uliopitiliza, uvutaji bangi, matumizi ya dawa za kulevya.

Kwa mujibu wa ubalozi huo, wanafunzi hawakuweza kuendelea na masomo kwa kipindi cha miaka miwili kutokana na lockdown iliyokuwa nchini China kutokana na maambukizi ya Uviko-19.

Amesema tayari wanafunzi waliokwama, wameanza kupokea barua za wito wa kurejea vyuoni na wengine wameshaanza michakato ya kurejea

Akitoa ujumbe maalum kwa wanafunzi leo Ijumaa, Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki, amesema wanafunzi wawasiliane na vyuo vikuu, hususani ofisi za kimataifa, ili kupata maelezo juu ya kanuni na masharti ya ukaazi wanayotakiwa kuyazingatia katika miji na vyuo vyao.

Balozi huyo alisema, tangu kutokea kwa mlipuko wa Uviko-19 mambo mengi yamebadilika nchini China, hivyo ni vyema wakafahamu mapema, ili kujiepusha na changamoto zinazoweza kujitokeza.

“Kwa mfano, kila anayeishi  China hivi sasa anatakiwa kuwa na kitu kinachoitwa namba ya utambulisho wa hali ya afya, ambayo anatakiwa aipakue kwenye simu yake na health code hiyo ndo inamruhusu mtu kuingia sehemu mbalimbali za umma, ikiwemo kuingia vyuoni,  mabwenini, hospitalini, madukani, kwenye mgahawa nk.

“ Bila namba hiyo huruhusiwi kuingia kokote kupata huduma,” alisema Balozi Kairuki.

Alisema kwa sasa, kila mtu anayeishi China anatakiwa kupima Uviko 19 kila baada ya siku tatu, zikipita siku tatu health code yake haitamuwezesha kupata kibali cha kuingia sehemui yoyote ile ya umma.

Katika hatua nyingine amewaasa wanafunzi kuishi katika hosteli za chuo, ili kuepukana na usumbufu unaoweza kutokea endapo watapanga nyumba mitaani.

“Wanaopenda kwenda kuishi mitaani kwa kisingizio cha kutafuta unafuu wa gharama mara nyingi wanajikuta wanaingia kwenye matatizo na kwa mazingira ya sasa ya China mitaani, ikitokea mtu mmoja amekutwa na Uviko-19 mtaa mzima unaenda lockdown siku saba, au zaidi.

“Kwa kufanya hivyo mwanafunzi anayekaa mtaani hataweza kuingia darasani kuendelea na masomo. Wanafunzi watambue manufaa ya kuishi hostel katika kipindi hiki,” alionya Balozi Kairuki.

Pia amewataka wanafunzi hao kuachana na aina zote za unywaji pombe uliopitiliza, uvutaji bangi, matumizi ya dawa za kulevya na kutojihusisha na wizi na utapeli, huku akisisitiza kuwa vitendo hivyo ni sababu kubwa zinazowakwamisha baadhi kuendelea na masomo na wengine kurudishwa nyumbani.

Habari Zifananazo

Back to top button